Na WAF, Gaborone – Botswana
Tanzania yaunga mkono kuwa na mifumo himilivu ya Afya na hasa Afya ya msingi ambapo ni lazima kuwa na Bima ya Afya kwa wananchi ili kuwapa uwezo wa kupata huduma bora wakati wote na kuondoa changamoto ya kutoweza kupata huduma pale wanapohitaji kwa sababu ya gharama.
Hayo ameyasema leo Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiendelea kushiriki mkutano uliyowakutanisha Mawaziri wa Afya kutoka Nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Àfrika mjini Gaborone, Botswana.
“Nchi za Afrika zimekubaliana ili kuwa na mifumo himilivu ya Afya na hasa Afya ya msingi ni lazima kuwa na Bima ya Afya kwa wananchi ili kuwapa uwezo wa kupata huduma bora wakati wote na kuondoa changamoto ya kutoweza kupata huduma pale wanapohitaji kwa sababu ya gharama”, amesema Waziri Ummy.
Aidha, Mkutano huo unaendelea kujadili ajenda nyingi na moja ya ajenda iliyojadiliwa leo kwa msisimko mkubwa na washiriki ni ajenda ya kuweka na kuimarisha mifumo himilivu ya huduma za Afya kwa wote barani Afrika.
Katika kikao hicho Waziri Ummy amechangia kuhusu ajenda hiyo na ameeleza kuwa, Tanzania inaunga mkono mpango wa huduma za Afya kwa wote katika Bara la Afrika ambapo ameshauri kuwa, Azimio la kuwa na mifumo himilivu katika utoaji wa huduma za Afya na Usalama limekuja wakati muafaka.
Pia, Waziri Ummy amesema katika kutekeleza mpango huu Tanzania kupitia mpango mkakati wa Sekta ya Afya wa Tano imeweka suala hilo kuwa ni kipaumbele kikubwa na ameridhia utekelezwaji wa mkakati huu.
Wakichangia mada hiyo, Mawaziri wa nchi mbalimbali wamesema kuna changamoto ya kutoimarishwa kwa Afya ya msingi katika nchi zote za Afrika ambapo imechangia vifo vya akina mama wajawazito kwa takribani 67% katika nchi zote za Afrika.
Hivyo, wameshauri kuwa, nchi za Afrika ziongeze upatikanaji wa rasilimali fedha ili kuongeza uwekezaji katika eneo hili.