Na Philipo Hassan – Arusha.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara – TANAPA Herman Batiho, amepokea Hati na Medali kutoka kwa wanachama ambao ni askari wastaafu waliopigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia (1939 – 1945) kwa kutambua mchango mkubwa uliotolewa na TANAPA katika kufanikisha tamasha lililokonga nyoyo na kuvuta hisia za watanzania la kumbukizi ya miaka 75 tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1939 hadi 1945, tamasha lililofanyika Dodoma tarehe 28.10.2021.Hafla hiyo fupi ya mapokezi ya hati na medali hizo yamefanyika leo tarehe 29.08.2023 katika Ofisi za Makao makuu ya shirika jijini Arusha.
Kamishna Batiho aliwapongeza mashujaa hao kwa kuwa mstari wa mbele kuipambania dunia, pia kwa kutambua mchango wa TANAPA katika kufanikisha tamasha hilo. Hata hivyo Kamishna hakusita kutoa pongezi za kipekee kwa Omary Shangali askari shujaa aliepigana vita vya pili vya dunia mwenye umri wa miaka 104 akiwa katika siha nzuri huku akipanda ngazi na kushuka bila shida wakati wa kukabidhi Medali na Hati hizo katika Ofisi za TANAPA.
Hata hivyo, Omar Shangali askari mstaafu machachali na mcheshi aliupongeza uongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kutunza Maliasili za nchi kwa ajili ya manufaa ya kizazi hiki na kizazi kijacho, na alilitaka shirika hilo lisiyumbishwe katika kulinda na kusimamia maliasili za nchi.