Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma amesema Wizara kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iko katika mkakati wa kuziendeleza fukwe za Kunduchi na Kigamboni katika Jiji la Dar es salaam kwa lengo la kukuza mchezo wa Soka la Ufukweni.
Naibu Waziri Mhe. Mwinjuma ameyasema hayo leo Agosti 30, 2023 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kawe, Mhe. Askofu Josephat Gwajima aliyetaka kujua lini Serikali itakuja na Mpango wa kuitumia Bahari kwa Michezo mbalimbali ya majini ili kuongeza kipato cha wananchi katika Jimbo la Kawe.
Amesema tayari TFF wameshaanzisha Ligi iliyoanza Agosti 19, 2023 ambayo hufanyika siku ya Jumamosi na Jumapili katika fukwe za Koko na jumla ya timu 16 zinashiriki ligi hiyo.
Mheshimiwa amelieleza bunge kuwa mwezi Julai, 2023, Timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni ilishiriki mashindano ya mchezo huo Barani Afrika iliyofanyika nchini Tunisia na kushika nafasi ya tatu, nyuma ya Morocco na Senegal.
Hivyo ametoa rai kwa wadau wa michezo mingine kama Mitumbwi na Ngalawa, Kuogelea, Mpira wa Kikapu na Wavu kuwekeza katika michezo hiyo ya ufukweni na kuziendeleza fukwe zilizopo ili kukidhi matakwa ya michezo yao kwani pamoja na kuongeza kipato kwa wananchi, michezo hiyo pia inasaidia kuimarisha afya na kutoa burudani kwa wananchi.