Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akisalimiana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), Bi. Sarah Gordon-Gibson walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) Bi. Sarah Gordon-Gibson akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo yaliyofanyika jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) Bi. Sarah Gordon-Gibson katika picha ya pamoja
….
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amemhakikishia ushirikiano Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), Bi. Sarah Gordon-Gibson.
Balozi Dkt. Shelukindo ametoa ahadi hiyo alipokutana na Bi Gibson aliyemtembelea Ofisini kwake jijini Dodoma.
Katika mazungumzo yao viongozi hao wamejikita katika kuimarisha ushirikiano na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano.
Balozi Shelukindo ameeleza kuwa Tanzania inatambua mchango mkubwa unaotolewa na WFP katika ukanda wa Afrika na Tanzania katika utekelezaji wa vipaumbele vyake.
“Tanzania chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua mchango wa WFP hivyo, itaendelea kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya kitaifa na kikanda.” Alisema Dkt. Shelukindo.
Naye Bi. Sarah ameeleza kuwa katika mpango mkakati wa miaka mitano (5) (2022-2027) Shirika hilo limejielekeza katika usaidizi wa masuala ya kibinadamu kwa wakimbizi waliopo Kigoma, shughuli za maendeleo kwa nchi ya Tanzania na Watanzania kwakuwa ongezeko la idadai ya watu kupitia uwepo wa wakimbizis linaathiri mfumo wa nchi katika namna mbalimbali.
Maeneo mengine ni pamoja na kujenga uwezo katika mpango wa tahadhari za kukabiliana na majanga, vifaa vya TEHAMA, lishe kwa jamii hususan katika uzalishaji wa vyakula na uelewa juu ya lishe bora ili kuondoa utapiamlo na usaidizi wa wanawake na watoto.
Kadhalika, WFP imeweka mkazo katika kilimo cha mahindi, maharage na mtama, kuongeza maeneo mapya ya usaidizi katika uzalishaji wa maua, matunda na mbogamboga na kujenga uwezo katika kukuza mnyororo wa thamani wa mazao ya chakula na biashara kuanzia kwenye uzalishaji hadi usambazaji kupitia bandari za Dar es Salaam, Kigoma na Mwanza.
“WFP imeweka mpango wa kushirikiana na Shirika la Reli (TRC) nchini ili kuwezesha kuwa na vituo vya ukusanyaji wa vyakula na kuwezesha usafirishaji wa vyakula hivyo kwa walengwa.
WFP kwasasa ina ofisi katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na inatarajiwa kufungua ofisi mpya mkoani Arusha.