Wakulima wa zao la chai nchini wahamasishwa kujitokeza kwa wingi ili katika mkutano wa AGRF ili waweze kunufaika na fursa za masoko zitakazotokana na Mkutano Mkubwa wa Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF).
Bi. Kemilembe Kafanabo, Mkurugenzi wa Huduma na Usimamizi bodi ya chai amesema kuwa Bodi hiyo inaendelea kuhamasisha wazalishaji wa chai kuzingatia matakwa ya vyeti vya ubora (Rainforest Alliance, Sustainable Agriculture, Fair Trade na viwango vingine vya kimataifa).
Bi. Kafanabo ameeleza kuwa Bodi ya Chai kwa kushirikiana na wadau muhimu imeendelea na maandalizi ya uanzishwaji wa mnada wa chai wa kidigitali utakaokuwa, jijini Dar es Salaam.
Vilevile, Bodi inaendelea kusajili wanunuzi wa chai kutoka nje ya nchi ambao wameanza kushiriki katika mnada huo ulioanza shughuli zake mwishoni mwa mwezi Mei, 2023.
Kuhusu vipaumbele vya kuchochea uzalishaji na mauzo ya zao la chai, Bi. Kafanabo amefafanua kuwa moja ya kipaumbele kilichowekwa ni kuhamasisha, kusimamia na kudhibiti uzalishaji ili kuongeza ubora wa chai unaokidhi viwango vya soko.
“Mkutano wa Mifumo ya Chakula Barani Afrika (African Food System Forum) unaleta shauku na hamasa kubwa kwa wazalishaji na wauzaji wa chai kupata taarifa mbalimbali zitakazochochea zao hilo kupata mapato zaidi,” amesema Bi. Kafanabo.
Aidha, uzalishaji wa zao la chai umeongezeka kutoka tani 24,825 kwa mwaka 2021/2022 hadi kufikia tani 26,754 kwa mwaka 2022/2023 na jumla ya tani 21,091 zimenunuliwa nje ya nchi. Huku vijana na wanawake wakiwa wanufaika zaidi katika ajira zitokanazo na kilimo cha chai.
Mkutano wa Jukwaa la AGRF umepangwa kufanyika tarehe 05 – 08 Septemba 2023, jijini Dar es Salaam.