Na Sophia Kingimali
Kuelekea mkutano mkuu wa mifumo ya chakula Afrika AGRF wafanyabiashara wamehimizwa kushiriki ili kuchangamkia fursa zitokanazo na mkutano huo kwani wafanyabishara wakubwa wa pembejeo wa kimataifa wanatarajiwa kushiriki.
Akizungumza wakati akifuatilia maandalizi ya mkutano katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere(JNICC) Agosti 29 jijini Dar es salaam katibu mkuu wa wizara ya kilimo Gerald Mweli amesema kupitia mkutano huo nchi itanufaika kwa kufikia mpango wa kulisha dunia pamoja kuuza mbolea ndani na nje ya nchi.
“lengo letu ni kuwa kitovu cha chakula si kuilisha tu nchi bali kulisha dunia katika mkutano huu wa AGRF tumealika makampuni yote makubwa hii itatoa fursa kwa wafanyabiashara wetu nchini kutangaza biashara zao kimataifa lakini pia kujifunza”amesema
Aidha mweli ameongeza kuwa nchi inatarajia kufungua kiwanda cha kuchakata mbolea kwa ajili ya kuuza ndani na nje ambapo kupitia AGRF nchi inategemea kukitangaza kiwanda hiko ili kupata masoko kimataifa.
Akizungumzia mkutano katibu mkuu amesema zaidi ya maraisi wanne wamekubali kushiriki akiwemo raisi wa kenya Wilium Ruto huku mawaziri wakiwa zaidi ya asilimia 80 ambao wakubali kushiriki na bado zoezi linaendelea.
Amesema mpaka sasa nchi imeshavuka lengo la washiriki ambapo washiriki walitakiwa 3000 lakini mpaka sasa wamezidi na kuweza kufikia 4000 hivyo wanatarajia kufunga dirisha la usajili leo agosti 29.
“idadi hii ya washiriki inaonyesha Imani yao kwa nchi yetu lakini kufikia jitihada hizo ni juhudi za raisi Dkt Samia Suluhu Hassani kuitangaza nchi kimataifa hivyo nitoe rai kwa watu wote wakiwemo wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mkutano huu wa AGRF kwani watapata manufaa makubwa”Ameongeza Mweli
Mkutano wa jukwaa la mifumo ya chakula kwa nchi za Afrika AGRF unatarajiwa kufanyika jijini Dar es salaam kuanzia septemba 5 mpaka 8 huku fursa nyingi zikitegemewa kupatikana hivyo ni nafasi kwa wafanyabiashara na wakulima nchini kushiriki