Na Sophia Kingimali
Ikiwa zimebaki siku chache kuelekea kwenye mkutano mkubwa wa jukwaa la mifumo ya chakula Afrika AGRF Wataalamu wa zao la Mpunga na wadau wa uzalishaji Mpunga (RBI) wa nchi za Afrika Mashariki na Kusini wamekutana kujadili changamoto na kutoa tathmini za utafiti wa kuendeleza zao la mpunga katika nchi hizo.
Akizungumza leo Agosti 28 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa wadau wa zao la Mpunga kutoka nchi 11 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli amesema washiriki wa uzalishaji Mpunga wataleta mkakati wa kuboresha uzalishaji wa zao hilo kwa nchi za Afrika Mashariki na Kusini.
Amesema Tanzania itakuwa na nguvu kubwa katika kuendeleza zao la mpunga kama mazao muhimu ushirikiano wa wakulima na taasisi za utafiti haswa TARI na mashirika ya kimataifa umekua kichocheo kikubwa.
“Tanzania kwenye takwimu zinaonyesha inashika nafasi ya pili Afrika kwa kuzalisha zao la Mpunga ikiwa inaongoza Madagascar hivyo Taasisi ya Utafiti wa Mpunga Kimataifa (IRRI) imeona Tanzania ina eneo lenye rutuba hivyo ardhi yake inafaa Kwa kuzalisha mpunga zaidi,”amesema Mweli.
Amesema zao la mpunga ni chakula na ni biashara soko lake la ndani na nje ni kubwa hivyo uzalishaji unapaswa. Kuongezeka ili kufikia lengo.
“Serikali ina pigania mabadiliko katika matumizi ya mpunga Kwa kutumia teknolojia ya kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mpunga. Kutoka chini ya tani 2.5 kwa hekta hadi tani tano au zaidi ifikapo mwaka 2030,” amesema.
Amesema lengo la serikali kuzalisha mpunga wa kutosha kukidhi mahitaji ya kitaifa kuchangia katika kula na usalama wa chakula kote Afrika na kuwa mzalishaji namba moja wa mpunga Barani.
Aidha amesema kwa programu ya RBI ni ushirikiano wa sekta muhimu na binafsi uliolenga kula na kutumia aina bora za mpunga kwa wakulima wadogo katika Afrika Mashariki na Kusini .
Mweli anasema Tanzania ina jukumu kubwa kama mzalishaji mkuu wa mpunga na mipango inatekelezwa na IRRI.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dk. Geoffrey Mkumilo amesema katika mkutano huo wanatarajia kuja na mikakati mikubwa kwa nchi Kwani ardhi yake inafaa kuzalisha Kilimo cha umwagiliaji na mvua.
“Tanzania ni nchi moja wapo ya wazalishaji wakuu wa mpunga Afrika lakini bado kuna nafasi kubwa ya kuboresha kiwango chetu cha wastani wa tani 2.5 kwa hekta ni eneo ambalo linahitaji umakini wa kitaifa, kikanda na kibara,”amesema Dk. Mkumilo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kikanda wa IRRI Afrika, Dk. Abdelbagi Ismail amesema Tanzania na nchi nyingi za Afrika Mashariki na Kusini kuchochea maboresho katika uzalishaji wa mpunga ili kupambana na njaa, umaskini wa kipato kwa mamilioni ya wakulima wadogo.
Amesema mpunga ni chakula lakini pia ni biashara na ni uhai kwa mamilioni watu hivyo wana jukumu la pamoja la kubuni na kuongeza uzalishaji wake na kuwa endelevu.
“Naamini kwa pamoja tunaweza kutimiza mengi zaidi na kuleta tofauti ambayo hakuna mmoja wetu angeweza kufanya pekee yake tuendelee na ushirikiano huu mzuri ,”amesema Dk. Ismail.