Makamu Mwenyekiti wa kamati kudumu ya bunge Katiba ,Utawala na sheria Mhe. Florent Kyombo akizungumza wakati alipotembelea Tume hiyo jijini Arusha.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Profesa Lazaro Busagala akizungumza katika kikao jijini Arusha.
Julieth Laizer, Arusha .
Kamati ya kudumu ya bunge Katiba ,Utawala na sheria imeishauri serikali kuendelea kuwekeza zaidi katika Tume ya nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) kwa kutoa elimu kwa zaidi kwa wananchi na kuongeza watumishi katika eneo hilo ili afya ya watanzania iendelee kuimarika.
Hayo yalisemwa jijini Arusha na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo ,Florent Kyombo wakati kamati hiyo ilipotembelea Tume hiyo kwa lengo mahususi kama mwendelezo wa elimu ambayo inaendelea kutolewa na Tume hiyo.
Aidha alisema kuwa,Rais Samia Suluhu Hassan amejitahidi sana katika kutoa fedha kwa ajili ya kuendeleza Tume hiyo ambayo imeweza kuwa na vifaa vya kisasa na vyenye ubora wa hali ya juu,huku wakiomba kuendelea kuwepo kwa uwekezaji zaidi kwani kinasaidia sana katika maswala mbalimbali.
Kyombo alisema kuwa, mnamo 28/6 walipokea muswada uliotumwa bungeni kwa mara ya kwanza muswada ambao ni wa sheria mbalimbali no 2/2023 mbapo miongoni mwa sheria sita ambazo zinarekebishwa ndani ya muswada huo mojawapo ni sheria ambayo inaigusa Tume hiyo.
Aliongeza kuwa, baada ya kupokea muswada huo bungeni wakiwa kama wajumbe ilionekana ni bora tupate uelewa kutoka Tume hiyo na kuweza kujizatiti zaidi katika ushauri kuhusu muswada huo.
“Baada ya kutembelea Tume hii leo mimi pamoja na kamati yangu tumepata elimu ya kutosha ambayo itasaidia sana kupanua uelewa na kuutendea haki muswada huo uliowasilishwa bungeni.”alisema Kyombo.
Aliongeza kuwa, wameweza kupata elimu sahihi na kujionea kuhusu vifaa mbalimbali ambavyo vinatumia mionzi ambavyo vimekuwa vikiratibiwa vizuri na wamejionea jinsi ambavyo Tume hiyo imejipanga katika kusimamia maeneo ya mipaka yote Tanzania na wataalamu wao wapo huko na wanaidhinisha kila kitu kinachoingia katika nchi yetu.
Kyombo alisema kuwa, Tume hiyo wamekuwa wakikagua vifaa vya X ray katika hospitali kama vinakidhi mahitaji na kutoa elimu mbalimbali ya matumizi hayo ,hivyo tunaomba waendelee kutoa elimu zaidi.
“Hata hivyo baada ya kutembelea Tume hii imekuwa na maombi mbalimbali kwa kamati hii ikiwemo kuomba sheria ibadilike katika swala la utoaji wa adhabu kwani hapo mwanzo ilikuwa ukiingiza kifaa ambacho kina mionzi kinyume na taratibu unaishia kufungiwa tu na hiyo haitoshi ,hivyo bunge litaenda kutunga sheria sasa na kupigwa faini kubwa ambayo itasaidia kuingizia serikali fedha nyingi kwa ambao wanaingiza vifaa kinyume na taratibu.”alisema Kyombo.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi hiyo ,Profesa Lazaro Busagala aliema kuwa kamati hiyo wametembelea kwa lengo la kuwajengewa uwezo wa vitendo katika ulinzi wa mionzi na matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia.
Alisema kuwa, baada ya kujengewa uwezo huo wataweza kuishauri bunge zima kwa ajili ya kuhakikisha watanzania wanafaidika kutoka na teknolojia ya nyuklia na watu waendelee kuwa salama zaidi ili madhara yanayoweza kujitokeza yasijitokeze.
Profesa Lazaro alisema kuwa, changamoto iliyokuwepo ni mwitikio mdogo wa watu wanaowasimamia kwani kuna wakati wanachelewa kuomba leseni na wakati mwingine wanachelewa kutekeleza yale ambayo wameelekezwa na wao kama Tume wanajikuta hawana nguvu za kisheria za kumshughulikia, hivyo kama wabunge wataridhia na kupitishwa maombi ya mabadiliko ya sheria wanaamini changamoto hiyo itaisha.
Naibu katibu mkuu wizara ya elimu sayansi na Teknolojia James Mdoe alisema pamoja na kamati hiyo kutembelea Tume hiyo na kuona namna ya utendaji wa kazi, ni wakati wa wabunge kuwaeleza wananchi katika maeneo yao juu ya elimu ya matumizi sahihi ya vyanzo vya mionzi na madhara yake pindi mionzi hiyo itakapotumika kinyume pasipo kufuata taratibu.
Mbunge wa jimbo la Kiteto ,Edward Ole Lekaita alisema baada ya kupata uelewa wa kutosha na kuondoa hofu waliyokuwa nayo wataenda kuwa mabalozi wazuri na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mionzi mbalimbali kwani wamegundua haina athari yoyote na kuwahakikishia kuwa wapo salama.