Naibu Waziri Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathewwakati akiongea na waandishi wa Habari Mara baada ya kufungua kikao cha 41 cha Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU) linaloendelea Jijini Arusha
Na Ahmed Mahmoud
SERIKALI ipo mbioni kuimarisha huduma za mawasiliano nchini, kwa kuweka mtandao wa Intaneti wa bure (WIFI) kwenye mikusanyiko yote, vyombo vya usafiri na kwenye shule, ili kila mwananchi apate huduma hiyo bila usumbufu wowote.
Akizungumza jana jijini Arusha, Naibu Waziri wa habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Methew Kundo, wakati akifungua kikao cha 41 cha Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU), alisema kikao hicho, kimefanyika ikiwa ni mfululizo wa vikao vyao, kwa ajili ya kuandaa ajenda ya pamoja kwa nchi za Afrika, ili kuziwasilisha katika kikao cha Baraza la Posta Duniani kitakachokaa Oktoba mwaka huu.
Mhandisi Kundo alisema uwekaji huo wa Intaneti za bure, zitasaidia wananchi kupata huduma za mawasiliano popote wanapokuwa na kuendelea na shughuli zao za kijamii, bila mkwamo wa ukosefu wa huduma hiyo.
“Hapa tunataka hakikisha umoja huu tunaboresha mifumo ya utendaji kazi na kua ya kidijitali na sisi kama Tanzania tukiwa wanachama wa umoja huu Afrika na Duniani, tumeanza fanya vizuri kwa kuanza na utekelezaji wa makubaliano, tuliyojiweke kwenye umoja wetu wa Afrika na Duniani, kwa kuweka sawa sera yetu ya posta ya mwaka 2003 kwa kuboresha miundombinu ya mawasilino,”alisema
Alisema mojawapo ya maboresho hayo ni ujenzi wa minara, mkongo wa Taifa na uwekaji wa Anuani za Makazi, ili kuhakikisha shughuli zote za posta zinafanyika vizuri na wananchi wanapata huduma za kijamii bila usumbufu.
Aidha, alisema Rais Samia Hassan Suluhu mwaka jana Februari 8 alihakikisha Tanzania kunakua na Anwani za makazi na hilo lilifanyika kwa ufanisi, ambapo kwa sasa kila mmoja anaona faida yake katika upatikanaji wahuduma za kijamii na hata potsa inakua rahisi.
“Zamani mtu ukikosea Anwani ya mtu kifurushi au barua inapotea inaenda mkoa mwingine, lakini sasa haiwezi kutokea kitu kama hiko, hivyo hii ni hatua kubwa tumepiga, kuelekea tunakotaka katika uimarishaji wa mawasiliano nchini,”alisema
“Tunavyoelekea kutoa huduma zote kidijitali ni lazima kuhakikisha uwezo wetu kimtandao unakua imara ili ifike mahali, kila mmoja asione umuhimu wa kutembea na fedha tasilimu, bali kadi tu na kupata kila aina ya huduma mtu anayohitaji kupata,”alisema
Alisema lengo lao kubwa kupitia PAPU nchi zote za Afrika, zitembee pamoja na iwepo nchi yoyote itakayobaki nyuma kwenye utoji wa huduma za mawasiliano
Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la PAPU,Richard Ranarison, alisema umoja huo unakusudia kutoa huduma bora na kwa wakati kwa kila nchi na ili kufikia lengo hilo, kila wanapokutana kwenye vikao vyao vya kila mwaka wanaangalia wapi walipo na wanapoelekea na penye dosari wanazirekebisha.