Na. Zillipa Joseph, Katavi
Katika kutekeleza kampeni ya upandaji miti, kwa lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yanayo sababishwa na uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli za binadamu, halmashauri ya Mpimbwe iliyopo wilayani Mlele mkoani Katavi imepanda miti 7,000 katika katika shamba lililotolewa na wananchi wa kijiji cha Ntibili kilichopo katika kata ya Kasansa.
Shughuli hizo ni pamoja na ufugaji wa kiholela, ukataji wa miti hovyo, uharibifu katika vyanzo vya maji, uchomaji wa misitu na kilimo kisicho na tija.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na halmashauri hiyo kupitia mradi wa urejeshaji endelevu wa mazingira na hifadhi ya bayonuai Tanzania, ya mwaka 2022/23 kijiji kilitoa shamba lenye ukubwa wa ekari saba kwa ajili ya upandaji wa miti hiyo.
Aidha katika kutekeleza kampeni ya upandaji miti, halmashauri imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa uhifadhi wakiwemo TFS, TAWA, hifadhi ya Taifa ya Katavi na mradi wa TASAF na LCMO.
Mpaka sasa shamba hilo limegharimu kiasi cha shilingi 31,936,080. Miti iliyopandwa katika shamba hilo ni pamoja na mitiki myeupe, mijohoro, mijakaranda na migunga.
Pamoja na faida zilizotajwa za uwepo wa shamba hilo ni huduma kwa jamii yenye uhitaji wa mazao ya misitu kama mbao, dawa, kuni, na kulinda chanzo cha maji cha Kifunda pamoja na kulinda msitu wa kijiji wa Masatu wenye ukubwa wa hekta 732.24.
Akiwa katika kijiji hicho kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa ndugu Abdalla Shaib Kaim na timu yake walijiunga na wananchi mbalimbali pamoja na wanafunzi kuendelea kuotesha miti katika shamba hilo.
Akizungumza mara baada ya zoezi la upandaji wa miti katika shamba hilo kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa bwana Abdalla Shaib Kaim aliwataka wananchi wa kijiji hicho kuacha kufanya shughuli za kuharibu misitu na vyanzo vya maji.
Ameonya juu ya tabia ya kuingiza mifugo katika vya maji na kufanya kilimo hadi katika maeneo ya karibu na vyanzo vya maji na badala yake amewataka kulinda vyanzo vya maji kwa umbali wa mita 60.