Viongozi na Maafisa wa manunuzi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya leo wameanza mafunzo ya siku tano yaliyotolewa na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Mbeya ambayo yamelenga kuwajengea uwezo washiriki juu ya taratibu sahihi za manunuzi za umma, ili kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika kwa ufanisi na kwa mujibu wa kanuni na taratibu za manunuzi.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa mafunzo, Dkt. Godlove Mbwanji Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya amesema kupitia mafunzo hayo yatawajengea uwezo washiriki kufahamu taratibu sahihi za manunuzi za umma, Sheria na kanuni za manunuzi pamoja na usimamizi wa mikataba ya umma ili kuhakikisha kuwa hospitali inaendesha manunuzi yake kwa uwazi, ufanisi na kuzingatia viwango vya ubora na usalama.
“Uongozi wa hospitali umeonelea tupatiwe mafunzo haya sisi sote ili yatusaidie kuimarisha uwezo wetu katika taratibu za manunuzi za umma ili kusaidia kuokoa fedha za umma na kuwezesha taasisi kutimiza majukumu kwa ufanisi zaidi katika kufanya manunuzi kwa kuzingatia kanuni na taratibu za manunuzi. Kuzingatia taratibu sahihi za manunuzi kutaimarisha uadilifu na ufanisi katika taasisi na hivyo kuongeza imani ya umma kwa taasisi za Umma.” – Dkt Mbwanji.
Naye Dkt. Elimeleck Parmena Akyoo Meneja wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Mbeya amepongeza Uongozi wa hospitali kwa uamuzi wao wa kuelekeza mafunzo hayo kutolewa viongozi na idara tumizi za hospitali ili kuboresha utendaji wa taasisi hiyo. Amesisitiza kuwa mafunzo hayo yatatoa fursa kwa washiriki kujifunza zaidi na kubadilishana uzoefu na wataalamu wenzao pia wameahidi kuendelea kutoa msaada na ushauri kwa washiriki baada ya mafunzo kukamilika ili kuhakikisha kuwa wanatumia ujuzi walioupata kuboresha utendaji.
“Nimefurahishwa sana na Uamuzi wa Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya kutoa mafunzo haya kwa Viongozi na Idara tumizi za hospitali. Hii ni hatua muhimu kuboresha utendaji wa taasisi ya umma na kuhakikisha kuwa taratibu sahihi za manunuzi zinafuatwa. Mafunzo haya yatawapa washiriki fursa nzuri ya kujifunza na kubadilishana uzoefu na wataalamu wenzao. TIA itahakikisha kuwa tunatoa msaada na ushauri kwa washiriki baada ya mafunzo kukamilika ili kuhakikisha kuwa wanatumia ujuzi walioupata kuboresha utendaji wao.” – Dkt. Akyoo
Naye mratibu wa mafunzo kutoka TIA Ndugu Muriano Nyandwi amesema lengo la mafunzo hayo ni kumwezesha kiongozi wa umma kufanya maamuzi sahihi ya manunuzi kupitia mafunzo hayo, na watahakikisha washiriki wanapata elimu ya kina kuhusu taratibu sahihi za manunuzi za umma na kusaidia kujenga uwezo wa washiriki katika kufanya manunuzi yenye tija.
Kupitia mafunzo haya, Viongozi mbalimbali wa hospitali wakiwemo Wakuu wa Idara na Vitengo, Wajumbe wa bodi ya zabuni, Kamati ya bajeti, Kamati ya dawa na Idara tumizi watajifunza na kubadilishana uzoefu na wataalamu wenzao, pamoja na kupata msaada na ushauri baada ya mafunzo ili kuhakikisha wanatumia ujuzi walioupata kuboresha utendaji wao katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.