Dkt. Venance Mwasse Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini STAMICO wakati wa Mkutano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, STAMICO na wahariri wa Vyombo vya habari katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC)
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Bw. Deodatus Balile akizungumza katika kikao hicho kati ya Msajili wa Hazina na STAMICO kilichofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere JNICC jijini Dar es Salaam.
Dkt. Venance Mwasse Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la STAMICO akiwa ameketi Meza kuu pamoja na baadhi ya wakurugenzi wa shirika hilo wakati Mkutano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, STAMICO, na wahariri wa Vyombo vya habari katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC)
Geofrey Meena Meneja Masoko na Mawasiliano STAMICO pamoja na maofisa wa shirika hilo wakiwa katika kikao hicho.
……………………………
*Yajipanga kuwainua wachimbaji wadogo
Na. Beatrice Sanga MAELEZO
Shirika la Madini Nchini (STAMICO) limesema litaendelea kusimamia shughuli zake kikamilifu ili kuongeza tija katika shughuli zinazotokana na madini, ikiwemo uchimbaji, uuzaji na kuongeza thamani madini mbalimbali.
Hayo yamesemwa Agosti 28, 2023 na Dkt. Venance Mwasse Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo wakati wa Mkutano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, STAMICO, na wahariri wa Vyombo vya habari katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) ambapo amebainisha kuwa kwa sasa Shirika hilo linasimamia miradi mbalimbali ikiwemo, Mradi wa Kiwira wa uchimbaji, uchakataji na uuzaji wa makaa ya mawe Mkoani Songwe.
Aidha ameeleza kuwa,miradi mingine inayosimamiwa na Shirika hilo ni pamoja na Mradi wa Mkaa Mbadala wa kupikia kwa kutumia makaa ya mawe, Mradi wa Dhahabu STAMIGOLD unaomilikiwa na serikali kwa hisa asilimia 99 na Msajili wa Hazina hisa asilimia 1 pamoja na kiwanda cha kusafisha Dhahabu Mwanza ambacho kinamilikiwa na Shirika hilo kwa asilimia 25 na Mbia asilimia 75.
“Uanzishwaji wa kiwanda hicho umesaidia, kusafisha dhahabu na mazao ambatano, uhaulishaji wa Teknolojia, kuongeza huduma kwa Jamii (CSR), mapato kwa serikali, STAMICO, na Serikali za Mitaa, kuongeza ajira, kupunguza utoroshaji wa dhahabu,
kutambulika kimataifa na kuimarisha Shilingi ya Tanzania na Uchumi.” Amesema Dkt. Mwasse
Mkurugenzi huyo pia amebainisha kuwa kwa sasa Shirika hilo limeongeza thamani yake na kuwezesha Taasisi mbalimbali zilizo chini yake kuendelea kufanya vyema kutokana na usimamizi mzuri wa sera na miongozo mbalimbali ya serikali kuhusiana na sekta ya madini.
“STAMICO Kutoka Shirika linalotengeneza hasara hadi Shirika linalotengeneza faida, tumeweza kulipa gawio kwa serikali jumla ya Shilingi Bilioni 8, tumeondokana kabisa na utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini, tumepata hati safi kwa miaka 3 Mfululizo kutokana na ukaguzi wa Mahesabu, lakini pia Mapato ya ndani yameongezeka kutoka Shilingi Bilioni 1.3 kwa Mwaka 2018/19 hadi Shilingi Bilioni 61.1 kwa mwaka 2022/23.” Amefafanua Dkt. Mwasse.
Vilevile amesema kwa sasa STAMICO imeendelea kuwainua wachimbaji wadogo kwa kuwafundisha mambo mbalimbali yanayohusiana na uchimbaji, ikiwemo masuala ya kisheria, na teknolojia.
“Tulifanya utafiti kwa wachimbaji wadogo na kubaini wana changamoto mbalimbali zikiwemo, elimu ya uchimbaji, ukosefu wa taarifa sahihi za mapato, Teknolojia duni, kutokuwa na mitaji/kutokukopesheka, na ukosefu wa masoko ya bidhaa zao.”, hivyo basi Shirika limeanzisha vituo vya mfano vya kujifunzia teknolojia vyenye tija ya uchimbaji katika maeneo ya Lwamgasa, Katente na Itumbi, pia tumeongeza uwezo wa kutoa huduma katika vituo hivyo na kutekeleza makubaliano (MOU) na Taasisi za kifedha CRDB, NMB, AZANIA na KCB ili ziweze kuwakopesha mitaji wachimbaji wadogo na kuwawezesha safari za kujifunza ndani na nje ya nchi. Amesema Dkt Mwasse
Aidha STAMICO kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), wameingia makubaliano ya awali na Kampuni za GF Truck na Apolo ili kuwawezesha kupata Vifaa kutoka kwa kampuni wauzaji wa Mitambo ya uchimbaji madini.
Mbali na mafanikio hayo Shirika hilo pia limepata Tuzo mbalimbali zikiwemo Tuzo 5 kwa mwaka 2023, ambazo ni pamoja na tuzo ya Taasisi ya umma iliyofanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji na yenye tija kwa mwaka 2023, Shirika la umma ambalo limetoa gawio kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, Mshindi wa Tuzo ya Kampuni ya Madini Bora ya Mwaka 2023 (ACOYA), Tuzo ya Uwezeshaji Wachimbaji Wadogo pamoja na Tuzo ya Mdhamini wa Maonesho.
Mbali na hayo, STAMICO imejipanga kuhakikisha kuwa ifikapo 2024/2025, kuondokana kabisa na Utegemezi wa Mishahara kutoka serikalini, kuongeza gawio lake serikalini, kuzalisha kwa wingi mkaa mbadala wa Rafiki briquettes unaotokana na Makaa ya Mawe, kuimarisha uchimbaji mkubwa wa makaa ya Mawe, kuongeza uwekezaji wake kwenye tasnia ya Uchorongaji, kuendeleza leseni za Shirika na kuzitangaza kwa lengo la kupata wawekezaji wa madini ya kimkakati ya Lithium, graphite, REE na Copper pamoja na kutekeleza mpango wa mafunzo (Training calendar) kwa ajili ya kuelimisha wachimbaji mikoa yote nchini.