Mkuu wa wilaya ya Same Kasilda Mgeni ametoa mwezi mmoja kwa uongozi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kuhamisha Gulio linalofanyika Jumatano hadi Jumapili eneo lililotengwa kwa ajili ya Viwanja vya Michezo Maarufu Kwasa-kwasa na kusababisha malalamiko kwa wanamichezo ambao wanashindwa kutumia eneo hilo.
Ameeleza pia kutoridhishwa na hali ya Soko kuu la Mji wa Same kutokana na Uchafu uliokithiri, Vyoo vinavyotumika kukosa ubora unaohitajika hivyo kuhatarisha usalama wa wafanyabiashara na wanunuzi wanaotumia Soko hilo na kuagiza halmashauri kukarabati vyoo vinavyotumika Sokoni hapo kufikia Septemba ya mwaka huu 2023.
Ametoa maagizo hayo wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Soko hilo ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi wa wilaya ya Same ambapo amesisitiza uboreshwaji wa miundombinu kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara.
Awali wafanyabiashara wa Soko kuu la Mji wa Same wakitoa malalamiko yao wamemweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa Soko hilo linakabiliwa na ubovu mkubwa wa miundombinu, uwepo wa mashimo makubwa yaliyo ndani ya Soko pia kukosekana nishati ya Umeme hali inayosababisha kuendesha biashara kwa shida wakitaharisha pia usalama wao.