Baraza la Wazee Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro wameeleza kuridhishwa na utendaji wa viongozi wa serikali wilayani humo hasa katika usimamizi wa Miradi ya maendeleo na kuboresha huduma pia kutafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali ikiwemo mapambano dhidi ya biashara haramu ya Dawa za kulevya.
Wakizungumza wakati wa hafla iliyoandaliwa na Baraza hilo maalum kumpongeza mkuu wa Wilaya hiyo ya Same Kasilda Mgeni Wajumbe wa Baraza hilo wamesema kwa muda mfupi tangu kuteuliwa kwake kuwa mkuu wa Wilaya ya Same kiongozi huyo ameonesha Ushupavu,Ujasiri na uhodari kwenye uwajibikaji kwa kuchukua hatua stahiki kwa wakati.
Mwenyekiti wa Baraza hilo la Wazee Timoth Mgonja amesema kilichowasukuka kuandaa hafla ya kumpongeza mkuu huyo wa Wilaya ni kutokana na mambo mbalimbali aliyokwisha yasimamia katika kipindi cha muda mfupi tangu kuteuliwa kwake.
“Tumefurahishwa kwanza na kitendo cha mkuu wa Wilaya kutukusanya wakati wa funga ya waislam, alituita wote bila kujali dini na kwa kauliyake mwenyewe akasema nimeona tufuturu pamoja kwasababu Serikali ya Same haina Dini watu wa Same ndio wenye Dini zao maneno yale yalitubariki sana”. Alisema Mwenyekiti wa Baraza la Wazee.
“Tuliona pia mambo mengine ikiwemo kupambana na taasisi inayohamasisha mapenzi ya jinsia Moja suala ambalo kwetu sisi Wapare ni uchafu uliopitiliza, lakini wakati huo huo tulikua tunaona Watoto wanaangamia kwenye madawa ya kulevya nako tukamuona huko Milimani anapambana kwenye Mirungi mpaka wakateketeza zaidi ya Ekari 500 hakika hapa tumepata kiongozi”.Alisema Mwenyekiti huyo wa Baraza la Wazee.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya hiyo Kasilda Mgeni ameshukuru hatua hiyo ya Baraza la Wazee kutambua kazi zinazofanyika wilayani humo, akiwaomba kuendeleza ushirikiano huo pia kwenye mambo mbalimbali ikiwemo kuhamasisha shughuli za maendeleo.
Amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassani inatambua umuhimu wa kundi hilo la Wazee kwenye ushiriki wao kuhamasisha shughuli za maendeleo, suala ambalo ndio kipaumbele chake akiahidi kuendeleza kuwashirikisha katika kila hatua kuweka urahisi kwenye kutafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali na kuendelea kuboresha upatikanaji wa Huduma.