Waganga Wakuu wa Mikoa nchini wametakiwa kuhakikisha wanawajengea uwezo wa utendaji kazi watumishi wa sekta ya afya hususani walio katika ngazi za chini ili kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Dkt. Wilson Charles Mahera wakati wa semina ya waganga Wakuu wa Mikoa iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI jijini Dodoma.
Dkt. Mahera amesisitiza kuwa, Waganga Wakuu wa Mikoa hawana budi kuwapatia ujuzi watumishi wanaowasimamia badala ya kusubiri uongozi wa juu kuandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji watumishi hao.
“Tunajua kuwa kuna changamoto ya kiutendaji kwa baadhi ya watumishi wa wa afya nchini hivyo madaktari bingwa nendeni kwenye vituo vya afya kuwafundisha kazi watumishi hao au wachukueni watumishi hao hata kwa wiki moja katika hospitali zenu ili wapate ujuzi,” Dkt. Mahera amesisitiza.
Aidha, Dkt.Mahera amekemea tabia ya wizi wa dawa na vifaa tiba na kuonya kuwa watumishi watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni zao.
Akizungumza kwa niaba ya Waganga Wakuu wa Mikoa, Dkt. Best Magoma ambaye ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ameiomba Serikali kuendelea kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya afya ili kuwawezesha watumishi kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Tunaomba kupatiwa magari ya kubebea wagonjwa na ya usimamizi, tunaomba ruzuku kwa ajili ya kuendeshea hospitali na vituo vyetu vya afya na tunaomba shuguli za lishe na ustawi wa jamii zipewe kipaumbele,” Dkt. Magoma amesisitiza.
Semina hiyo ya siku 2 imelenga kuwajengea uwezo kiutendaji Waganga Wakuu wa Mikoa ili kuboresha utendaji wao kazi na kuleta matokeo chanya katika sekta ya afya.