Timu ya mpira wa miguu ya kata ya Nyasaka imefanikiwa kuifunga timu ya kata ya Ilemela goli moja kwa sifuri, Goli lililofungwa dakika ya 23 na mchezaji Mathias James katika uwanja wa Sabasaba wilayani Ilemela.
Akizungumza wakati wa mchezo huo Mgeni rasmi ambae pia ni diwani wa kata ya Kirumba Mhe Wesa Juma amesema kuwa anamshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa kuanzisha mashindano hayo yenye lengo la kukuza viwango vya mpira wa miguu.
‘.. Namshukuru sana Mbunge Dkt Angeline Mabula kwa kutuletea mashindano ya Jimbo Cup, Kupitia mashindano haya tutakuza vipaji vyetu ..’ Alisema.
Aidha Mhe Wesa amewaasa wachezaji hao kutokuwa sababu ya kutia dosari mashindano hayo pamoja na kuwataka kuweka mbele maslahi ya wengi, upendo na umoja Ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kufikiwa.
Kwa upande wake nahodha wa timu ya kata ya Nyasaka Bwana Boaz Sagelo mbali na kumshukuru Mungu kwa ushindi walioupata ameongeza kuwa timu yake imejipanga vizuri kuhakikisha inashinda michezo yote iliyosalia huku akiwaomba mashabiki kuendelea kuiunga mkono Ili iweze kuchukua ubingwa wa mashindano hayo.
Nae mchezaji wa timu ya kata ya Ilemela Bwana Salehe Kakombe amesema kuwa timu yake ilicheza vizuri na ilifanikiwa kutengeneza nafasi nyingi za kushinda Ila wameshindwa kuzitumia hivyo wataenda kujipanga kwaajili ya mchezo unaofuata.
Mashindano ya The Angeline Jimbo Cup 2023 yataendelea kutimua vumbi hapo kesho katika viwanja vinne vya Baptist Kona ya Bwiru, Bugogwa shule ya msingi, Sabasaba na Buswelu shule ya sekondari.