Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amawataka wajasiriamali kurasimisha biashara zao ili waweze kufanya biashara kwa wigo mpana zaidi.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo tarehe 24 Agosti, 2023 katika ufunguzi wa Kongamano la Wanawake na Ununuzi wa Umma lililoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Ng’arisha Maisha Foundation Jijini Tanga, lenye lengo la kutoa mwamko kwa wajasiriamali ili waweze kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana baada ya kurasimisha biashara zao.
Ameongeza kuwa ili kwenda na wakati na kupata fursa zinazotokea katika mchakato mzima wa ununuzi ni vyema wajasiriamali wakarasimisha biashara zao ili kuwa miongoni mwa watakaopata zabuni.
“Natambua kuwa mmekuwa mkiandaa bidhaa bora na wengine mkiwa na huduma ambazo kwa namna moja au nyingine mnapaswa kupata zabuni ila pasipo kurasimisha biashara zenu BRELA na taasisi nyingine itakuwa ni vigumu kupata nafasi hizi, hivyo mfike kurasimisha biashara zenu”, amesema Dkt. Gwajima.
Kwa upande wake Afisa Usajili kutoka BRELA Bw.Abdul Songolo akifafanua kuhusu huduma zinazotolewa na na Taasisi katika Kongamano hilo amesisitiza kuwa milango ya kufungua biashara ipo wazi na BRELA imerahishisha huduma kwani wanaweza kujisajili mahali popote walipo kupitia mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS).
Amesisitiza kuwa BRELA inaendelea kuwasogezea wadau huduma ikiwa ni pamoja na kuwafikia mahali popote ili kutoa mafunzo na huduma za papo kwa papo.
Wajasiriamali zaidi ya 1,000 wamehudhuria Kongamano hilo na kuonesha mwitikio mkubwa katika kuchangamkia fursa hasa za kusajili biashara zao.