Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga akizungumza wakati wa Mkutano wa Msajili wa Hazina, TTCL na Wahariri wa vyombo vya habari katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Leo Alhamisi 24,2023.
Deodatus Balile Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) akitaka ufafanuzi katika baadhi ya mambo katika kikao hicho.
Mkurugenzi wa Huduma ya T-Pesa, Lulu Mkudde kutoka shirika la mawasiliano TTCL akifafanua jambo katika kikao hicho.
……………………..
*Mkongo wa taifa wanufaisha nchi Zaidi ya 4
Na Beatrice Sanga-MAELEZO
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limejipanga kuhakikisha kuwa uchumi wa kidijitali unafikiwa hapa nchini ili kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, hivyo limejipanga kufikia mwaka 2024 kila wilaya itakuwa na huduma ya mtandao yenye kasi na ubora katika kurahisisha shughuli mbalimbali za uzalishaji mali pamoja na za kijamii.
Hayo yamesemwa Agosti 24, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga wakati wa Mkutano wa Msajili wa Hazina, TTCL na Wahariri wa vyombo vya habari katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), ambapo amebainisha TTCL itahakikisha inaendelea kuwa kitovu wezeshi cha uchumi wa kidijitali nchini.
Mhandisi Ulanga amesema kuwa kwa sasa Shirika hilo limeanza kwa kuboresha kasi ya mtandao kwa kusambaza mkongo wa Taifa katika wilaya mbalimbali nchini na vilevile linatoa huduma za fibre mlangoni ambazo zitahakikisha wananchi wote wanapata mtandao wa kasi zaidi nchi nzima.
“Tumeanza kupandisha uwezo wa mkongo wa Taifa kuanzia gigabyte 200 kwenda gigabyte 800 na tunatarajia ifikapo mwezi Januari 2024 tutafika terabyte 2 ambayo ni uwezo mkubwa kabisa, lengo kubwa ni kuhakikisha wananchi wanapotumia huduma za mtandao ziwe za gharama nafuu, lakini vilevile ziwe zinafika mahali mbalimbali, ifikapo Januari 2024 tutakuwa tumefikisha wilaya 100, lakini lengo letu ifikapo Desemba 2024 tutafikia wilaya zote 139,” amesema Mhandisi Ulanga.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa shughuli mbalimbali zitakuwa zinafanyika kwa njia ya mtandao ikiwemo ufundishaji, matibabu katika sekta ya afya, kuongeza miamala kwa njia za mitandaoni ambapo amesema kwa sasa huduma za kifedha kwa njia ya kidigitali bado hazifanyiki kwa kiwango kikubwa kutokana na changamoto mbalimbali ambazo kwa sasa zinafanyiwa kazi.
“Hilo lina faida tatu kiuchumi moja, litaweka rekodi sahihi za matumizi ya fedha maeneo mbalimbali, mbili litarahisisha uwezo wa kukopa na kupeleka miamala sehemu mbalimbali na la tatu litaweza kuleta huduma mbalimbali za kifedha kama vile bima kwa urahisi na nafuu kwa watumiaji wote,” alisema.
Aliongeza kuwa, changamoto ambazo zimekuwa zikikwamisha utekelezaji wa sera ya uchumi wa kidijitali ikiwa ni pamoja na miundombinu tayari zimeanza kufanyiwa kazi na wamejipanga kufikia 2025 uchumi wa kiditijali utakuwa umefikiwa nchi nzima kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Deodatus Balile ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) amesema kuwa serikali imenuia kuimarisha sekta ya mawasiliano ili kukuza uchumi wa kidigitali nchini, hivyo ameiomba kuendelea kuwahabarisha wananchi juu ya mambo mbalimbali yanayofanywa hususani katika mabadiliko ya Mashirika na Taasisi za umma kwa ushirikiano na vyombo vya habari pamoja na wahariri.
“Kama tunataka kujenga Taasisi ambazo zitakuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi, lakini pia zikaenda kama tulivyoona TTCL inavyowezesha karibu nchi zote zilizotuzunguka, kama Burundi, Kenya, Zambia, sehemu nyingi zinawezeshwa na mkongo wa TTCL, basi ni lazima tufike mahali kwamba hizi Taasisi za umma ziwe na uwezo wa kufanya uamuzi, uamuzi wa kibiashara na zisijifungie ndani kama alivyosema Mheshimiwa Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan,” alisema Balile.
Mkutano huo wa Shirika la Mawasiliano Nchini umefanyika ikiwa ni mwendelezo wa Mikutano ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, Wahariri wa vyombo vya habari pamoja na Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za serikali zilizo chini ya ofisi hiyo ikiwa ni katika kuelezea mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kutokana na shughuli zinazofanywa na Taasisi hizo.