Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha leo Agosti 24, 2023 limepokea msaada wa vifaa vya michezo ambavyo ni jezi seti mbili na fedha taslimu 1,500,000/= kwa ajili ya Timu ya Polisi ya Netbal mkoani hapa inayojiandaa kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Muungano.
Kamanda wa Polisi Mkoani hapa Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo wakati akipokea vifaa hivyo vilivyotolewa na kampuni ambazo ni Joagro Safaris, Luna Safaris, na Avinta Care Clinic mbali na kushukuru kwa msaada huo, pia amesema vifaa hivyo vitakua ni chachu kwa timu hiyo kufanya vizuri zaidi katika michuano iliyopo mbele yao.
ACP Masejo amebainisha kuwa michezo ni sehemu ya kuwaleta watu karibu na Jeshi la Polisi hasa katika kufikisha ujumbe kwa jamii kuhusiana na suala zima la ulinzi na usalama hali inayopelekea kuwa na ushirikiano mzuri na wananchi.
Kwa upande wa wadau waliotoa vifaa hivyo wamesema wanaunga juhudi za Jeshi la Polisi katika kuzuia na kudhibiti matukio ya uhalifu Mkoani hapa ambapo jamii inaendelea na shughuli zake za kiuchumi katika hali ya amani na utulivu.
Sambamba na hilo pia wamesema ni utaratibu waliojiwekea wa kurudisha kwa jamii kutokana na faida walizozipata kupitia shughuli zao na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa mara kwa mara kwa Jeshi hilo.
Jeshi la Polisi linashiriki michezo mbalimbali kupitia mradi wake wa Polisi jamii ujulikanao kwa jina la mpango wa michezo kwa vijana katika kuzuia na kupambana na uhalifu.
Lengo la mradi huo pamoja na mengine ni kujenga ushirikiano na mahusiano mazuri baina ya Jeshi la Polisi na jamii katika kupata taarifa mbalimbali za kihalifu sambamba na utoaji wa elimu ya usalama.