NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA
MATOKEO chanya ya kuongezeka kwa mpato yameanza kuonekana katika Halmashauri za Wilaya za Kwimba,Misungwi na Sengerema, kufuatia uchambuzi wa mfumo wa kukusanya mapato uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza.
Pia malalamiko 57 kati ya 70 ya vitendo vya rushwa yaliyotolewa na wananchi katika kipindi cha Aprili hadi Juni,2023 yanachunguzwa na taasisi hiyo huku ikishinda kesi mbili kati ya tatu zilizotolewa hukumu na mahakama.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza,Idrisa Kisaka, amesema leo kuwa katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2023 walichambua mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya madini ya ujenzi (mchanga,kokoto,changarawe na mawe)na kubaini mianya ya upotevu katika halmashauri za Wilaya za Misungwi,Kwimba na Sengerema.
Amesema mianya hiyo ilisababishwa na halmashauri kutokutenga maeneo ya uchimbaji wa madini hayo,kukosa taarifa ya fedha zinazokusanywa katika chanzo hicho,wafanyabiashara kutokuwa na leseni wala vibali na wakandarasi waliotekeleza miradi ya maendeleo kutokulipa ushuru.
Pia baadhi ya halmashauri hazikuwa na chazo hicho katika mashine zao za kukusanyia mapato (POS),ama ziliweka watumishi wachache na kusababisha ufanisi mdogo na hivyo mapato hayo yaliwanufaisha zaidi wenyeviti wa vitongoji na vijiji badala ya halmashauri.
“Tathmini tuliyofanya ya kuimarisha mfumo wa kukusanya mapato na kudhibiti rushwa katika madini ya ujenzi,mapato yameongezeka katika halmashauri hizo na kufikia sh.1,321,040,319.86 mwaka wa fedha 2022/23 kutoka sh.403,308,766.76 mwaka wa fedha 2021/22 kabla ya uchambuzi,”amesema Kisaka.
Amesema kuwa taasisi hiyo katika kipindi hicho cha Aprili hadi Juni, 2022/23 ilifuatilia miradi 25 ya maendeleo yenye thamani ya sh. 12,346,094,719.97 katika sekta za barabara,elimu,afya na maji.
Naibu Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoani humu amesema mradi wa Jiji la Mwanza wa ujenzi wa barabara za urefu wa km 2.64 kwa kiwango cha lami uliogharimu sh.1,481,496,358.24 walibaini kasoro ya kupasuka kwa kingo na mitaro,walishauri yafanyike marekebisho na mradi umekamilika.
Kwa mujibu wa Kisaka miradi tisa ya elimu,barabara na afya yenye thamani ya sh.3,459,753,527.24 imekamilika kati ya miradi 25 ya maendeleo ambapo miradi 16 ya elimu,afya na maji yenye thamani ya sh.8,886,341,192.73 inaendelea kutekelezwa mkoani Mwanza.
Pia upande wa uchunguzi na mashtaka amesema katika kipindi hicho cha Aprili hadi Juni,2023 walipokea taarifa 70 kati ya hizo 57 za vitendo vya rushwa zinachunguzwa huku mahakama ikitoa uamuzi katika kesi tatu ambazo Jamhuri ilishinda mbili huku kesi 14 zikiendelea kusikilizwa mahakamani.
Kisaka ameeleza moja ya majukumu ya TAKUKURU ni kudhibiti mianya ya rushwa katika taasisi za serikali na zisizo za kiserikali kwa kuchambua mifumo ya utendaji kazi, ikilenga kubaini mianya ya rushwa na kushauri watendaji namna bora ya kuhudumia jamii na kuepuka vitendo vya rushwa.