Na Shamimu Nyaki
Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imepokea na kujadili taarifa ya Mkakati wa Ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao hadi kukamilika kwake utagharimu Bilioni 31 na utafanyika kwa muda wa miezi 12.
Katika taarifa hiyo Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema uwanja huo mbali na kutumika katika mchezo wa Mpira wa Miguu pia umekua ukitoa huduma ambazo zimekua chanzo cha mapato kutoka Kwa wadau mbalimbali walioweka huduma zao ikiwemo mitambo ya Mawasiliano, kumbi 10 za mikutano pamoja na kutumiwa na nchi jirani ikiwemo Uganda Djibouti, Sudan na Burundi.
Naye Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amesema baada ya ukarabati huo Wizara itatoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi na utunzaji wa uwanja, usimamizi na udhibiti wa vitendo vya uharibifu wa miundombinu unaofanywa na baadhi ya watu huku akiiomba Kamati Iendelee kutoa ushirikiano Ili kufanikisha jambo hilo.
Awali akiwasilisha taarifa ya Mkakati huo kwa niaba ya Waziri, Katibu Mkuu wa wizara hiyo Bw. Saidi Yakubu amesema Ukarabati huo utahusisha eneo la kuchezea ambalo litafadhiliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) baada ya timu ya Simba kufuzu kucheza Afrika Football League, Benchi la Ufundi ambalo litafadhiliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF).
Eneo lingine alilosema Katibu Mkuu Yakubu litakalofanyiwa ukarabati ni eneo la mchezo wa Riadha, vyumba vya kubadilishia nguo vya wachezaji, kubadilisha viti vyote na kuweka vya kisasa ambavyo vitakua na namba na havitakua vinapigwa na jua moja kwa moja, chumba cha kisasa cha wanahabari, mifumo ya maji safi na majitaka, ubao wa matangazo, taa mpya za kisasa, mifumo ya umeme na mtandao pamoja na eneo la watu mashuhuri ambalo litawekwa viti visivyohamishika.
Wakichagia taarifa hiyo, Wajumbe wa Kamati wamepongeza hatua hiyo na kusisitiza ukarabati utakapokamilika kuwe na usimamizi madhubuti wa uwanja, kuwe na akaunti kwa ajili ya kuwekewa fedha za matumizi ya uwanja kwa ajili ya matengenezo madogo, ambapo pia wameshauri Serikali itoe fedha za usimamizi wa uwanja huo ambazo zimetengwa kwa wakati.
Akihitimisha kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Husna Sekiboko ameisistiza wizara kutoa elimu kuhusu matumizi ya fedha zilizotolewa za ukarabati wa uwanja huo, na kuweka utaratibu wa kukarabati uwanja huo mara kwa mara, ambapo pia ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa fedha hizo.