Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Bodi ya Utalii (TTB) ndiyo nguzo muhimu katika kutangaza na kuvutia watalii kutembelea Nchi yetu sanjari na kuongeza mapato yatokanayo na Sekta ya Utalii.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Bodi za Wakurugenzi za TTB na Hifadhi ya Taifa (TANAPA) uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa AICC jijini Arusha na kuitaka TTB kuanza mikakati ya kubaini fursa za uwekezaji kwenye utalii.
Amesema kuwa Serikali ipo katika kufanya mapitio ya sheria ambayo itawapa mamlaka TTB kuhakikisha kwamba wanaishauri vyema kwenye eneo la uwekezaji kwenye sekta ya utalii.
“TTB mtakuwa na kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha kuna nyongeza ya ujenzi wa hoteli mbalimbali, nyongeza ya vyumba na kufikiria kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ya ufukwe au kwenye visiwa” amesema Mhe Mchengerwa
Amesema kuwa kwenye suala la uwekezaji wanatambua hadi leo hii idadi ya vyumba vilivyopo nchini kwa ajili ya watalii ni ndogo sana ambavyo ni 120,000 ukilinganisha na nchi jirani ya Kenya yenye vyumba zaidi ya milioni 1,500,000.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTB Dkt Mohamed Dau amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani aliyoionesha na kumpa nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TTB.
Dkt. Dau amesema kuwa takwimu zinaonesha bara la Asia ndilo lina watu wengi ambapo kunahitaji kuweka mkazo wakutangaza Utalii kwenye Bara la hilo kwasababu huko ndiko watalii wengi wapo ili kuweza kuongeza idadi ya watalii kuja Tanzania.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Bw. Damasi Mfugale amesema TTB itaendelea kubuni mikakakati mbalimbali yenye lengo la kuimarisha uhifadhi, utangazaji na uendelezaji wa Sekta ya Utalii nchini.
Amesema kuwa mikakakti hiyo itazingatia mawazo na miongozo itakayotolewa na bodi za wakurugenzi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) ametoa pongezi kwa Mhe Rais katika kazi kubwa anayoifanya katika kulea uhifadhi na kutangaza Utalii na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Bodi za Wakurugenzi zilizoteuliwa ili ziweze kutimiza malengo ya Taifa na Taasisi zao.
Wakati huo huo, Bodi ya Utalii Tanzania imeaingia makubaliano ya ushirikiano na Kamisheni ya Utalii Zanzibar ikiwa na lengo la kuongeza ushirikiano wa kitengaji katika taasisi hizo.