Katika kuhakikisha elimu inaendelea kuchangia katika uchumi wa taifa, imeelezwa kuwa ni wakati sasa wa kufanyika kwa Mabadiliko ya Mitaala ya Elimu ya Vyuo Vikuu na vya Kati ili elimu inayotolewa na vyuo hivyo iweza kuendana na teknolojia inayotumiwa na viwanda katika shughuli za uzalishaji wa malighafi.
Akifungua kikao cha Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Mipango, Fedha na Utawala katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Amandus Muhairwa, amesema mradi huo umelenga kufanya maboresho ya sekta ya elimu katika vyuo vikuu na vyuo vya kati hapa nchini.
Amesema kwa Chuo hicho, mradi huo una thamani ya shilingi bilioni 73.6 ambao utaleta mageuzi makubwa katika uboreshaji wa miundombinu ya Ufundishaji na Ujifunzaji kwa wanafunzi wa Chuo hicho pamoja na wafanyakazi.
Prof. Muhairwa amesema uboreshaji wa mazingira ya huo utafanyika kwa kujenga madarasa mapya yenye ubora yatakayozingatia kwa wenye mahitaji maalum, kuboresha miundombinu ya maabara, mashamba ya mazao na wanyama ambayo yatakuwa katika viwango vya kimataifa.
“Tumekutana katika kikao hiki kujadili na kupata mrejesho wa mradi huu, kwa SUA pekee mradi unathamani ya shilingi bilioni 73.6, na tangu kuanza kwa mradi huu tumefanikiwa kupeleka takribani walimu 41 kwenda kusoma nje ya nchi na tumeshaandaa mikakati mingine ya kujenga madarasa, kuboresha miundombinu ya kufundishia ili kuleta mapindizu ya kiuchumi kupitia elimu” Amesema Prof. Muhairwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya uratibu wa uboreshaji na ukuzaji wa mitaala SUA Dkt. Jamal Jumanne, amesema kufanyika kwa Mabadiliko ya Mitaala ya Elimu kwenye Vyuo vikuu na Vyuo vya kati kunatazamiwa kuchochea kasi ya ukuaji wa Uchumi, endapo vyuo hivyo vitajikita katika utoaji wa elimu pamoja na mafunzo yenye ujuzi wa kuviwezesha viwanda kuongeza uzalishaji.
Naye Mratibu Msaidizi wa Mradi wa HEET katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Dkt. Winfred Mbungu amesema mradi huo unafadhiliwa kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia, ukitekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika Taasisi 22 hapa nchini, zikiwemo Taasisi 14 za Elimu ya Juu, Taasisi 5 zilizopo chini ya Wizara ya Fedha pamoja na Taasisi 3 zilizo chini ya Wizara ya Elimu.
Amesema mradi huo utaboresha na kuongeza ufanisi wa elimu itolewayo na vyuo vikuu pamoja kuimarisha usimamizi wa elimu ya juu hapa nchini, ambapo kwa SUA katika mitaala mipya wataenda kuimarisha mashirikiano na sekta binafsi vikiwemo viwanda pamoja na matumizi ya TEHAMA ili kuwawezsha wahitimu kuendana na kasi ya mahitaji ya viwanda, hatua ambayo itawaongezea ufanisi katika mageuzi ya kiuchumi.