Na Englibert Kayombo – WAF Tanga
Wito umetolewa kwa watanzania kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kutambua hali zao kiafya mapema na kuepukana na maradhi ambayo yanaweza kugharimu fedha nyingi za matibabu na hata kusababisha ulemavu hadi vifo.
Wito huo umetolewa leo na Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Mheshimiwa Ummy Mwalimu ambaye pia ni Waziri wa Afya nchini Tanzania alipokuwa akifungua kambi ya upimaji afya ya Afya Cheki iliyoandaliwa na Uongozi wa Afya Cheki kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Tanga na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
“Watanzania wengi tunakwenda Hospitali tayari ugonjwa umeshakuwa mkubwa sana, wagonjwa wa Saratani wanakwenda Hospitali, Saratani ikiwa hatua ya nne, hatuna mazoea ya kupima afya mapema kujua hali zetu” ameeleza Mhe. Ummy mwalimu kwa kutolea mfano wa hali ya ugonjwa wa Saratani.
Amesema kuwa maradhi yakigundulika mapema huwa ni rahisi kuyatibu lakini pia kupunguza madhara, hivyo kupitia kambi hiyo ya Afya Cheki anawahimiza, kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi wa Mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla umuhimu wa kupima afya. katika Taasisi ya Saratani ya Ocean ameshuhudia akiona wagonjwa wanafika wakiwa wanaugua Saratani ya tezi dume, Saratani ya Mlango wa Kizazi, ugonjwa umeshasambaa mwili mzima.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa ya upatikanaji wa huduma za afya nchini. “Huduma za matibabu ni gharama, wananchi wengi bado hawamudu gharama za matibabu, suluhisho pekee ni kujiunga na bima ya afya ili tuwe na uhakika wa matibabu pale tutakapokuwa tumeugua” aemesema Mhe. Ummy Mwalimu.
Kwa upande wake Mratibu wa AfyaCheki Dkt. Isack Maro amesema kuwa kazi hiyo wanaifanay kwa ari bila kushurutishwa kuwaelimisha na kuwahamasisha watanzania umuhimu wa kupima afya zao na kuweza kupata huduma za matibabu mapema.
“Kuna ongezeko kubwa sana la magonjwa hasa ya kuambukiza, magonjwa haya yanaanza taratibu bila dalili zozote na huonekana baadae yakiwa tayari yameshaathiri kwa kiwango kikubwa, hivyo tunawakumbusha wananchi kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa afya zao hata mara moja kwa mwaka na kutambua namna ya kuzuia magonjwa haya ya kuambukiza” amesema Dkt. Isack Maro.
Naye Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Riziki Kisonga ambaye pia ni Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma nchini amesema kuwa kupitia Kambi hii ya Afya Cheki Wizara ya Afya itashiriki katika kutoa huduma ili wananchi wa Mkoa huo na maeneo Jirani waweze kupata huduma za upimaji afya Jirani na maeneo yao.
“Wizara ya Afya kwenye kambi hii tumejipanga kutoa huduma ya upimaji wa ugonjwa wa kifua kikuu, maambukizi ya Viruisi vya Ukimwi, huduma za upimaji na utoaji wa dawa za Malaria pamoja na upimaji wa magonjwa yote yasiyokuwa ya kuambukiza” amesema Dkt. Riziki.
Kambi ya upimaji Afya kupitia kampeni ya Afya Cheki imeanza leo Agosti 21 na itakuwepo mpaka Agosti 25, 2023 ambapo wananchi wa Mkoa wa Tanga na maeneo Jirani wanakaribishwa kuja kupata huduma za upimaji afya bure bila gharama yeyote katika Viwanja vya Usagara.