Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) pamoja na Waumini wa Kanisa hilo, kwenye Maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Viwanja vya Mfuko wa Wastaafu Mkoani Arusha tarehe 21 Agosti, 2023
….
Julieth Laizer, Arusha .
Arusha .RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kuwa , kuhusu utekelezaji wa mkataba wa bandari wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai ameamua kunyamaza kimya na ataendelea kunyamaza kimya kwani hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuligawa Taifa hili.
Ameyasema hayo leo agosti 21 jijini Arusha katika maadhimisho ya miaka 60 ya KKKT katika Chuo kikuu cha Tumaini Makumira mkoni Arusha .
“Nimeyasikia yote uliyoyasema (Askofu Shoo) kuhusu usalama ,amani,umoja na mwendelezo wa Taifa letu,niliamua kunyamaza kimya na ninaendelea kunyamaza kimya.
“Ninachotaka kuwahakikishia ni kuwa hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuligawa Taifa hili,hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuharibu wala kuuza Taifa hili.”amesema Rais Samia.
Amesema ,viongozi wa dini ndio wenye jukumu la kukuza kusimamia na kutunza maadili yetu kama watanzania ili vijana wetu waishi maisha ya kumpendeza Mungu ,tuwakuze watoto wetu waishi maisha ya kumpendeza Mungu naomba viongozi wa dini wabebe jukumu hili kwa kiwango kikubwa.”amesema.
Samia amesema ameshuhudia namna ambavyo kanisa hilo wamekuwa wakitoa huduma mbalimbali za kiroho na kimwili kwa zaidi ya miaka 60 na leo ni maadhimisho ya kitaifa kwa kanisa hili ni jambo kubwa sana la kumshukuru Mungu.
Ameongeza,Serikali imekuwa ikishirikiana na Taasisi za kidini katika kutimiza wajibu wake ndo maana wote kwa pamoja wamekuwa wakishirikiana katika kuchangia maendeleo ya nchi
“Nawaahidi kuwa,Taasisi za dini zote serikali itaendelea kufanyia kazi changamoto zote zinazowakabili kwa ustawi wa maendeleo ya nchi yetu “.
Ameongeza ,kila mmoja wetu ni shuhuda kwa namna ya mabadiliko ya tabia ya nchi yanavyotokea kwa watu wa vizazi vyetu na hii ni kutokana na kuwa tumeacha kutunza dunia na kufanya mabaya,hivyo kuwataka kubadilika na kuyatunza mazingira yetu kwa manufaa ya nchi yetu kwa ujumla.
“Mazingira hayaachi kutuadhibu kama tunavyoyaharibu sisi naomba wote tukawe rafiki wa mazingira kwani uhifadhi wa mazingira ni jukumu letu sote na nawaomba sana Wananchi watumie vyanzo mbadala katika kukabiliana na mabadiliko hayo ya tabia ya nchi .”amesema Rais Samia.
Aidha amewataka wenye kanisa kujidhatiti kuendana na yale mabadiliko, huku akiwataka viongozi wa dini kudumisha umoja na sala ili nchi iweze kuishi kwa amani.
Amewapongeza kwa dhati viongozi waliomaliza nafasi zao na kuwaomba viongozi watakaochaguliwa kuendeleza misingi mizuri ya kanisa.
Naye Askofu Mkuu wa kanisa la KKKT ,Frederick Shoo amesema kuwa ,wao kama kanisani wanaunga mkono swala la uwekezaji katika Dp World na ya kuwa wao hawapingi uwekezaji kwani wanajua serikali inahitaji wawekezaji.
“Mheshimiwa Rais unakumbuka sisi viongozi wa dini tulikuomba kuja kuonana na wewe madhehebu yote ya kikristo ulitusikiliza na kupokea maoni yote na kuahidi kufanyia kazi kwa maslahi mapana ya Taifa.
“Tunakuamini katika jambo hili Mheshimiwa kuwa taasisi na vyombo vyake vitafanyia kazi jambo hili tena kwa umakini mkubwa .”amesema Askofu Shoo.
Askofu Shoo amesema , kupitia jambo hili kuna watu wanataka kugawanyika kabisa kwa sababu zao lakini wanamshukuru Mungu kama mama na kiongozi amekaa kimya,na jambo hili linahitaji umakini katika kuliendea jambo hili pasipo nchi kugawanyika.
“Kanisa lipo pamoja na tutaendelea kukuombea na kanisa litaendelea kuunga mkono kwa maslahi ya Taifa letu. “.
Kanisa litaendelea kusimamia haki za binadamu na kuheshimu mamlaka zilizopo jambo ambalo litaimarisha umoja wa kimataifa kwani kazi yetu kubwa ni kuwaombea kuhakikisha kila kitu kinaendea sawa.
“Hata tukipata sehemu ya kukemea tutakemea pia ila tunaomba tusiambiwe tunachanganya dini na siasa. “
Aidha Shoo amewataka Viongozi wa dini kutumia nafasi zao kulizungumzia swala la mabadiliko ya tabia ya nchi ili kunusuru nchi yetu huku akiwataka kujiingiza kwenye maswala ya nishati mbadala.
“Viongozi wenzangu na wanasiasa tuache kuwagawa watu kwa misingi ya kisiasa na kwa maslahi binafsi ,anayefanya hivyo kwa nia mabovu akemewe na asionewe aibu kabisa, na kanisa lipo tayari kuwa na serikali katika maswala mbalimbali .”.
Amesema kuwa, tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo mwaka 1963 walikuwa na waumini laki 5 ambapo kwa sasa wapo waumini milioni 8 na wana dayosisi 27 sasa na zingine zinaendelea kuzaliwa.
Amesema kanisa hilo limeenea katika mikoa yote ya Tanzania bara na tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo
limekuwa likitoa huduma za jamii katika kuhudumia kimwili na kiakili.
Ameongeza kuwa ,kumekuwepo na ushirikiano wa kutosha kwenye maswala ya elimu kwa kuwepo kwa shule zenye vipaji maalumu ambapo kanisa limetoa kwa serikali .
“Mimi nilikereka juzi kusikia mtu anasema kwa nini serikali inatumia fedha zake kusaidia Taasisi za dini na hiyo tunaweza kusema huyo mtu hajui historia ila ana sababu zake nyingine.”amesema .
Fedha zinazotokana na kusamehewa kwa taasisi hizo fedha hizo zishirikiane kuendelea kuchangia maendeleo na serikali kwani kuna baadhi ya wanasisiaa wanapiga vita swala hilo nafikiri ni vizuri tukaheshimu ushirikiano huo na asiwepo mtu yoyote wa kubeza ushirikiano huo katika ya serikali na taasisi hizo.
“Mheshimiwa Rais nakupongeza sana kwa kushika nchi na mimi nasema huu ulikuwa ni mpango rasmi wa Mungu nakuomba Mheshimiwa Rais ufanye kazi yako kwani Mungu ndo kakuweka kwenye nafasi hiyo na sisi tunaheshimu hilo watu ambao hawajaridhika na uwepo wako hadi sasa nawapa pole sana”
Amesema kuwa,uwepo wa mshikamano kwa wananchi wote katika kukuza uchumi wa demokrasia na uhuru wa kuongea,napongeza sana falsafa yako ya kukuza uchumi.