Na Sixmund Begashe
Makumbusho ya Dkt. Rashid Kawawa iliyopo Bombambili, Songea Mkoani Ruvuma imekuwa kivutio cha wengi kutokana na kubeba historia adhimu ya Waziri Mkuu wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. Rashid Mfaume Kawawa, ambaye pia alisimama kidete na Waasisia wenge kutafuta uhuru wa Tanzania awali Tanganyika.
Akizungumzia kuhusu Makumbusho hiyo Mhifadhi wa Makumbusho hiyo Bw. Danson Majogo amesema, uwepo wa Makumbusho licha ya kuchagiza maendeleo ya Utalii Kusini mwa Tanzania pia imetoa fursa kubwa Kwa wananchi kuongeza ufahamu juu mchango mkubwa wa Hayati Dkt. Kawawa nchini, Uzalendo, Uaminifu, Utu, Mshikamano wa Kitaifa.
“Makumbusho hii ikiyofunguliwa rasmi 2017 inasaidia sana Utalii wa ndani, imesheheni mikusanyo ya kipekee ya vitu vilivyotumiwa na Hayati Dkt. Kawawa maarufu kama “Simba wa Vita”, picha machapisho na vinginevyo vinavyompatia Mtalii nafasi licha tu ya kujifunza basi hata kuburudika”. Alisema Bw. Majogo
Naye Bi. Rehema Mbiro Mkazi wa Songea, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri ya Uhifadhi wa Historia ya Waasisi wa Taifa hili, Utangazaji vivutio vya Malikale jambo linalochochea ongezeko la Utalii wa ndani, huku akitoa wito Kwa watanzania kuitembelea Makumbusho hiyo kwa uwelewa mpana kuhusu Tanzania.