WAZIRI wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amebainisha maeneo ambayo yamelengwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya watoto (UNICEF) ili kuboresha Sekta ya Afya nchini ikiwemo eneo la afya ya uzazi, lishe na usafi.
Waziri Ummy amebainisha hayo leo Agosti 17, 2023 alipokutana na kufanya mazungumzo na mwakilishi Mkazi wa Shirika la Kimataifa-UNICEF Bi. Elke Wisch aliyeambatana na ujumbe kutoka Shirika hilo katika ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma.
Amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kutekeleza afua mbalimbali za kupunguza vifo vya watoto wachanga katika vituo vya kutolea huduma hasa kwenye zahanati kwa kujenga vyumba maalumu kwaajili ya huduma za watoto hao (Neonatal Care Unit)
Kwenye eneo la mapambano dhidi ya maambukizi ya Ugonjwa wa UKIMWI, Waziri Ummy amesema Serikali imeendelea kutekeleza Mpango wa 95-95-95 ili kuhakikisha inafikia malengo ya kuutokemeza ugonjwa huo ifikapo 2030, huku akisisitiza nguvu kubwa inawekwa kwenye kundi la mabinti balehe ambao ndio kundi linaloongoza kwa maambukizi.
Aidha, Waziri Ummy amesema Wizara yake inaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu ili kuweka mkakati mzuri utaoruhusu suala la afya ya uzazi kuwekwa katika silabasi ili wanafunzi wanufaike na elimu hiyo itakayosaidia kupunguza maambukizi ya magonjwa pamoja na mimba za utotoni.
Kwa upande wa Magonjwa Yasiyoambukiza(NCDs), Waziri Ummy amesema, jitihada za kuelimisha umma juu ya kufanya mazoezi na masuala ya ulaji unaofaa zinaendelea ili kukabiliana na magonjwa hayo.
Pia, amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanya kazi kubwa ya kupambana na changamoto ya lishe kwa watoto, ikiwemo kuingia mikataba na viongozi wa Mikoa ili kuondoa changamoto ya masuala ya lishe na udumavu kwa watoto hasa walio chini ya miaka mitano.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa UNICEF Bi. Elke Wisch ameipongeza Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa inayofanya katika kuboresha afya za wananchi, na kusisitiza UNICEF itaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali kupitia Wizara ya Afya ili kufikia malengo yake ya kuboresha huduma za afya kwa Watanzania.