Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewasilisha taarifa ya utendaji wa Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira.
Mhe. Aweso ameishukuru serikali kwa kuwezesha mfuko huo kwa sababu umesaidia kwa kiasi kikubwa kusukuma mbele maendeleo ya sekta ya maji. Amesema kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 Mfuko ulipokea jumla ya shilingi bilioni 137.5 ambazo zimewezesha utekeleza wa miradi 325 ya maji.
Ameongeza kuwa hadi mwezi Juni 2023 jumla ya miradi 62 imekamilika na inawanufaisha wananchi wapatao 2,155,756 na miradi 263 inaendelea na utekelezaji.
Ameihakikishia kamati hiyo kuwa lengo la serikali la kufikia asilimia 85 ya upatikanaji wa huduma ya maji vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2025 litafikiwa. Hadi sasa huduma ya maji imefikia asilimia 77 vijijini na asilimia 88 mijini.
“Tunashukuru kwa mawazo na michango mikubwa kutoka kwa wajumbe wa kamati, pia mshikamano mkubwa wa wataalamu wa Sekta ya Maji na viongozi wote” Mhe. Aweso ametoa shukrani hizo kwa Kamati ya Maji na Mazingira na ili kuongeza wigo wa mapato amesema wizara imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuanzisha dirisha la mikopo ya riba nafuu.
“Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) unaendelea kutafuta vyanzo vipya vya mapato ili kutunisha Mfuko ikiwa ni pamoja na kuanzisha dirisha la mikopo ya riba nafuu kwa Mamlaka za Maji hapa nchini na kufanya majadiliano na wadau wa maendeleo, pia kujenga uwezo wa Taasisi katika uandaaji wa maandiko ya miradi (water project proposals) ambayo yatatumika kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi.” Waziri Aweso amesema.
Ameongeza kuwa kwa sasa chanzo kikuu cha mapato ya mfuko ni tozo itokanayo na uuzaji wa mafuta ya petroli na dizeli kwa shilingi 50.
Eneo jingine ambalo limepewa kipaumbele na NWF ni utunzaji wa vyanzo vya maji ambapo kazi ya upandaji miti rafiki wa maji inafanyika, uwekaji wa mipaka na mabango kwenye vyanzo vya maji, utangazaji wa maeneo ya vyanzo vya maji kama maeneo tengefu, uchimbaji wa visima na ujenzi wa mabwawa sambamba na urejeshaji wa mito kwenye mikondo yake;
Mwenyekiti wa Kamati ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) na wajumbe wake wameipongeza Wizara ya Maji na kuitaka ihakikishe inafuatilia uendelevu wa miradi inayotekelezwa ikiwemo miti rafiki katika vyanzo vya maji. Pia kuweka nguvu katika kuongeza wigo wa ukusanyaji fedha ili kuharakisha utekelezaji wa miradi.
Mhe. Kiswaga ametoa heko hususani eneo la kazi mbalimbali kwa watumishi kufanya kazi kama timu pamoja na viongozi katika Sekta ya Maji. Amesema juhudi hizo zinaipaisha Sekta ya Maji na kufikisha huduma muhimu ya maji kwa jamii.