Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MBUNGE wa Simanjiro Mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka, amewaonya vijana nchini kutojiingiza kwenye uhaini na pia wasiunge mkono maandamano ya kupinga Serikali kupitia mitandao ya kijamii.
Ole Sendeka akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo, amewaasa vijana wa eneo hilo kutojiingiza katika kuunga mkono uhaini wowote nchini.
Amesema Serikali ina mkono mrefu katika kushughulikia amani iliyopo hivyo vijana wa eneo hilo wasijiingize kwenye uhasi au uhaini kwani watashughulikiwa na kujilaumu baadaye wakiwa wamechelewa.
“Ninampongeza mkuu wa jeshi la polisi nchini, IGP Camilius Wambura kwa kutoa onyo kupitia vyombo vya habari kuwa atawachukulia hatua watu au kikundi kitakachoandamana ili kuiangusha Serikali kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,” amesema Ole Sendeka.
Amesema endapo vijana watakuwa wanahitaji jambo lao, zipo njia mbalimbali za kudai haki zao kupitia mazungumzo na muhimili mwingine wa mahakama, kuliko kuunga mkono maandamano ya uhaini.
“Hata kwenye makundi yenu ya mitandao ya kijamii msijaribu kuingia kwenye mtego wa kuwaunga mkono watu wanaotaka kufanya uhaini kwani mtachukuliwa hatua kali za kisheria na kisha kujuta baadaye,” amesema Ole Sendeka.
Amewataka viongozi mbalimbali wa ngazi ya kata na vijiji, kuzungumza na vijana wa maeneo yao kuwa wasidhubutu kuunga mkono uhaini unaofanywa kupitia mitandao ya kijami.
Amesema suala la ubinafsishaji wa bandari limefika hadi kwenye mahakama hivyo ni jambo zuri na uamuzi umetolewa, endapo hawajaridhika wakate rufaa na siyo kufanya uhaini.
“Unapotaka kuunga mkono au kufanya uhaini kwa Serikali halali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan utakuwa unajitafutia matatizo, hivyo vijana epukeni,” amesema Ole Sendeka.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amemuunga mkono Ole Sendeka kwa kuwaasa vijana waepuke hayo na wafanye kazi ili kujiinua kiuchumi.
“Vijana mnapaswa kujitambua na kuepuka kujiingiza kwenye mambo ambayo hayana maana kwa mustakabali wa Taifa, kwani suala la kuunga mkono uhaini litawagharimu,” amesema Kanunga.