NA MWANDISHI WITU, DAR ES SALAAM.
Katibu wa Baraza la Habari la Kiislamu (BAHAKITA) Sheikh Said Mwaipopo amesema kuwa kitendo cha Jeshi la Polisi kuwakamata Boniphace Mwabukusi, Mdude Nyagali pamoja na Dkt. Wilbroad Slaa kumetokana na kutoa kauli za kuhamasisha uvunjifu wa amani na sio kuzungumzia uwekezaji wa bandari ya Dar es Salaam kama baadhi ya taasisi na wadau mbalimbali wanavyosema.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 17, 2023 Jijini Dar es Salaam,
Katibu wa Baraza la Habari la Kiislamu
(BAHAKITA) Sheikh Said Mwaipopo, amesema kuwa Dkt. Slaa, Mwabukusi, Mdude hawajakamatwa kwa sababu ya kuzungumzia mkataba wa bandari ya Dar es Salaam.
“Dkt. Slaa na Mdude wametoa kauli za kuhamasisha uvunjifu wa amani, walisema wataiwajibisha na kuipindua serikali, viongozi ni wezi pamoja na kuvamia vituo vya Polisi na ofisi za CCM” amesema Sheikh Mwaipopo.
Sheikh Mwaipopo amesema kuwa kauli walizotoa wanasiasa hao inatosha Jeshi la Polisi nchini kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria.
Amesema kuwa nchi ya Tanzania ina vyombo vya sheria, ulinzi na usalama pamoja na Jeshi la Polisi ambalo miongoni mwa majukumu yake ni kukamata, kuhoji na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa.
“Nimepata wasiwasi baadhi ya taasisi ambazo zinasimamia haki za binadamu wamasema sio haki kuwakamata, walivyosema wanavamia vituo vya Polisi na kuwakamata watu kuna mahusiano gani na masuala ya uwekezaji wa bandari ? ” amesema Sheikh Mwaipopo.
Amefafanua kuwa mkataba wa uwekezaji wa bandari hauna mahusiano yoyote na Jeshi la Polisi na CCM “Wanaojiita watetezi wa haki za binadamu, hizo haki zipo kwa waharifu tu, walitaka waachiwe ili wakachome moto vituo ya polisi na ofisi za CCM ?” amesema Sheikh Mwaipopo
“Hawa watu hawajakamatwa kwa sababu ya kupinga uwekezaji, wamekamatwa kwa maneno yao machafu ambayo hayavumiliki na serikali yoyote duniani”amesema Sheikh Mwaipopo.
Amesema kuwa serikali ipo sahihi kuwakamata kutokana na kauli zao, na kila mtanzania anayo haki wa kukemea vitendo ambavyo sio rafiki.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Mwabukusi na Mdude waliokamatwa Agosti 12 Mikumi Mkoani Morogoro na wanashikiliwa kwa tuhuma za kutoa kauli za uchochezi, huku Dkt. Slaa aliyekamatwa Agosti 13 jijini Dar es Salaam akishikiliwa kwa tuhuma hizo.