Na Selemani Msuya
NCHI za Afrika zimeshauriwa kuwekeza katika utafiti wa mbegu asili kwa kuwa zina lishe bora, uhakika wa chakula na salama kwa afya ya mtumiaji.
Ushauri huo umetolewa na wadau mbegu asili kutoka nchi 25 za Bara la Afrika, Marekani na Ulaya ambao wanakutana jijini Dar es Salaam kwa siku tatu kujadili hatma ya mbegu asili katika nchi zao na dunia kwa ujumla.
Akizungumza katika mkutano huo Paul Chilewa kutoka Mwamvuli wa Asasi za Kuendeleza Kilimo Hai Tanzania (TOAM), alisema mkutano huo ambao umehusisha zaidi ya watu 100 kutoka nchi 25 ni muhimu kwa wadau wote wa mbegu asili kujadiliana namna ya kuzilinda mbegu za asili.
Chilewa alisema Afrika kwa sasa ina changamoto kubwa ya mbegu za asili, hali ambayo itachangai kukosekana kwa uhakika wa chakula kwa siku nyingi.
“Mbegu asili zina lisha nyingi na salama kwa afya ya mtumiaji, hivyo ili kuhakikisha zinakuwa endelevu ni lazima kufanyika tafiti ambazo zitaonesha ni namna gani tunaweza kuzilinda,” alisema.
Ofisa huyo alisema iwapo Serikali itafanya utafiti ambao utashirikisha wakulima ambao wanatumia mbegu asili ni wazi kuwa changamoto hiyo itapata jibu sahihi.
Chilewa alisema iwapo hakutakuwa na juhudi za kukabiliana na changamoto ya mbegu asili, ni wazi kuwa wakulima wataingia kwenye mtego wa kununua mbegu ambazo zitahitaji viuatilifu na mbolea ambavyo vina sumu na kusababisha maradhi mbalimbali.
Mratibu wa Mratibu wa Mtandao Baionoai Tanzania (TABIO) Abdallah Mkindi alisema utafiti unaonesha asilimia 80 ya wakulima wa Afrika wanatumia mbegu asili, hivyo ni muhimu kuhamasisha matumizi ya mbegu hizo.
Alisema pia utafiti umeonesha mbegu asili zina virutubisho, hivyo iwapo jamii itahamasishwa kutumia mbegu hizo changamoto ya utapiamlo ambayo inakabili mataifa hayo itapata muafaka.
“Mbegu asili zina nafasi kubwa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yameonesha madhara makubwa duniani, hivyo rai yangu ni kuziomba serikali za Afrika kutenga fedha zitakazotumika kufanya utafiti wa mbegu hizi,” alisema.
Mkindi alisema TABIO kwa kushirikiana Mtandao wa Uhuru wa Chakula Dunia (AFSA) na SwissAid wamewakutanisha wadau hao ili waweze kujadiliana na kutoka na kauli moja kuhusu hatma ya mbegu asili ambazo zinaonekana kupewa kisogo na watunga sera na sheria.
Kwa upande wake Mbunge wa Lindi mjini, Hamisa Abdallah alisema kilimo cha mbegu asili ndio kinaweza kuleta tija kwenye sekta hiyo, kwani historia inaonesha wazee wa zamani walitumia njia hiyo.
Hamida alisema mbegu asili hazina gharama kwenye kilimo kama ilivyo kilimo cha kisasa, hivyo ni wakati muafaka wa jamii kurejea katika mfumo huo wa zamani.
Alisema kutokana na madhara ambayo yanapatikana kwenye kilimo cha kisasa, dunia imeanza kubadilika na kutaka kurejea mifumo ya zamani ambayo ilijikita katika mbegu za asili.
“Mimi naishi na wakulima wa hali ya chini ambao anashirikiana nao kuendeleza matumizi ya mbegu asili, hivyo anaungana na wadau wengine ambao wanataka uwekezaji katika utafiti wa mbegu hizo ambazo ni salama kwa afya ya binadamu,” alisema.
Alisema mkutano huo ni ujumbe sahihi kwa viongozi duniani kuweka mkazo wa kusisitiza kilimo kinachojikita katika mbegu asili ambazo ni salama kwa afya ya binadamu na mazingira.
Hamida alisema tafiti zinaonesha kuwa hata ongezeko la magonjwa dunia kwa sasa sababu kubwa ni jamii kuacha kutumia mbegu asili kwenye kilimo.
“Sisi Lindi tumefungua benki ya mbegu asili, hiyo ikiwa ni kuonesha ni namna gani tumejipanga kuachana na mbegu za kisasa ambazo zina madhara mengi kwenye afya ya binadamu,” alisema.
Mbunge huyo alisema atumia nafasi yake ya ubunge kuzungumzia na kushawishi umuhimu wa mbegu asili kwenye kilimo.
Mwakilishi wa Wizara ya Kilimo, Beatrice Banzi alisema Tanzania imekuwa ikihamasisha watafiti kufanya utafiti katika sekta hiyo ya mbegu asili na mbegu zingine.
Alisema kilio cha dunia ni uwepo wa mbegu bora na salama kwa afya ya binadamu, hivyo utafiti pekee ndio unaweza kutoa jibu.
Ofisa Program wa AFSA, Famara Diédhiou alisema ni wakati muafaka kwa nchi za Afrika kuungana kuhakikisha mbegu asili zinapewa kipaumbele katika sekta ya kilimo.
“Tumekutana hapa Tanzania nadhani ni wakati muafaka kwa sisi kupigania uwepo wa chakula bora chenye lishe, kwa kuhamasisha matumizi ya mbegu asili,” alisema.
Katika mkutano huo nchi zilizoshiriki ni Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia, Senegali, Burkina Faso, Ivory Cost, Hispania, Norway, Zambia, Zimbabwe, Australia, Togo, Mali, Benin, Chad, Tunisia, Niger, Afrika Kusini, Botswana, Malawi, Misri, Rwanda, DR Congo na Gabon.