Meneja Habari na Mawasiliano Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Muungano Saguya akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Shirika hilo Upanga jijini Dar es Salaam kuhusu madeni ya wapangaji wa nyumba za NHC , Kushoto ni Adolf Kasegenya Mkurugenzi wa Fedha NHC na katikati ni Elias Msese Mkurugenzi Usimamizi wa Miliki NHC.
Elias Msese Mkurugenzi Usimamizi wa Miliki Shirika la Nyumba NHC akifafanua jambo wakati wa mkutano huo, kulia ni Meneja Habari na Mawasiliano Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Muungano Saguya.
Meneja Habari na Mawasiliano Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Muungano Saguya akifafanua baadhi ya mambo katika mkutano huo kulia ni Elias Msese Mkurugenzi Usimamizi wa Miliki Shirika la Nyumba NHC na kushoto ni Adolf Kasegenya Mkurugenzi wa Fedha NHC.
……………………………….
NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM.
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeanza kuwachukulia hatua za kisheria wadaiwa sugu ambao kwa ujumla wao wanadaiwa shilingi bilioni 23 ambazo zingeweza kusaidia utekelezaji wa shughuli mbalimbali ikiwemo miradi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 15 /8/2023 Jijini Dar es Salaam, Meneja Habari na Mawasiliano Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Muungano Saguya, amesema kuwa wameanza kampeni ya kukusanya madeni yote kwa kipindi cha mwenzi mmoja.
Bw. Suguya amesema kuwa Kampeni hiyo imebeba kauli mbiu isemayo “Lipa Madeni yako Kwa Maendeleo ya Shirika letu na Taifa”.
Amebainisha kuwa miongoni mwa hatua ambazo wamechukua NHC ni kuingia mikataba na wapangaji ili waweze kulipa kwa awamu madeni yao pamoja na kuendelea kulipa kodi ya kila mwezi.
Amesema kuwa wapangaji wakishindwa kulipa kodi ya kila mwezi pamoja na madeni yao watavunjiwa mikataba, huku akieleza kuwa waliopewa notisi ya kuhama utekelezaji wake unaendelea.
Bw.Suguya amesema kuwa mpangaji mpya hatapangishwa bila kulipa dhamana ya pango kwa muda wa miezi mitatu pamoja na wapangaji wanaoendelea kuishi wanapaswa kulipa dhamana hiyo hadi kufikia Disemba 31, 2023.
“NHC imeingia makubaliano ya kupeleka majina ya wadaiwa sugu katika Taasisi za fedha ili wasipate huduma ya mikopo kutokana na kuwa sio waaminifu,
Shirika halitampa mkataba mpya mpangaji msumbufu katika kulipa kodi” amesema Bw. Suguya.
Hata hivyo amesema kuwa uongozi wa NHC imeunda kamati ya kufuatilia madeni yote na kuhakikisha wadaiwa walipa.
“NHC ilikuwa inadai bilioni 28 kutoka kwa wapangaji wake baada ya kuanza kuchukua hatua tayari Shilingi bilioni 5 zimelipwa na sasa zimebaki bilioni 23” amesema Bw. Suguya.