Na Mwanahamisi Msangi, MBEYA
SERIKALI ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo mstari wa mbele kuinua na kuimarisha uchimbaji wa madini ujenzi katika Mgodi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara Kongolo Quarry) kwa kuhakikisha inawawezesha mashine bora na za kisasa zikiwemo za uchorongaji, kuvunja na kusaga madini.
Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa Mgodi wa Tazara Kongolo Quarry, Iddy Abdallah, alisema kuwa mgodi unazalisha madini ujenzi ya aina tano tofauti yakiwemo mawe madogo kwa matumizi ya reli, kokoto za ujenzi wa barabara na mchanga kwa matumizi ya ujenzi wa majengo.
“Tunaishukuru sana Serikali chini ya usimamizi wa Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini kwa kuhakikisha inatupa mwongozo, lakini kubwa zaidi Mhe. Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kutuwezesha vitendea kazi kama mashine za kisasa na kutuahidi kuendelea kutuletea mashine mpya ili kuongeza ufanisi wa kazi katika mgodi wetu,”alisema Meneja.
Akifafanua zaidi Meneja wa Mgodi alisema kuwa katika kuzalisha mawe, mgodi unatoa bidha za ujenzi na mpaka sasa baadhi ya Taasisi za Serikali zinapofanya miradi ya kijamii zinanunua bidhaa za ujenzi katika mgodi huo.
“Mimi ni Meneja wa Saba tangu tuanze mgodi huu mwaka 1975 tunatoa ajira fupi fupi na wapo watumishi 72 ambapo kati ya hao raia wa kigeni ni mmoja, tunaiomba Serikali kuendelea kutuwezesha ili tuzidi kuongeza Pato la Taifa,”alisema Meneja Abdallah.
Naye Msimamizi wa uchimbaji wa madini ujenzi katika mgodi huo, Ndulupia Andondile, alisema kuwa kwa sasa wanafanya vizuri katika uchimbaji lakini bado wanahitaji zaidi fedha kwa ajili ya ununuzi wa baruti za kuvunjia miamba.