Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akimkabidhi zawadi inayotangaza bidhaa za Tanzania ikiwemo kahawa, korosho na mvinyo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Bima-SINOSURE ya China, Mhe. Song Shughuan, wakati wa Ziara ya kikazi ya Ujumbe wa Tanzania, Makao Makuu ya Taasisi hiyo mjini Beijing, ambapo Tanzania na Taasisi hiyo zimeingia makubaliano yatakayoiwezesha Tanzania kunufaika na huduma za dhamana inayotoa kwa Taasisi za Fedha za China zinazotoa mikopo ya aina mbalimbali hatua itakayoiwezesha nchi ikiwemo Sekta Binafsi, kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo na kiuchumi.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) upande wa kulia, akiongoza Ujumbe wa Tanzania, walipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Taasisi ya Bima ya China-SINOSURE, Makao Makuu ya Taasisi mjini Beijing-China, ukiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Song Shughuan, ambapo Tanzania na Taasisi hiyo zimeingia makubaliano yatakayoiwezesha Tanzania kunufaika na huduma za dhamana inayotoa kwa Taasisi za Fedha za China zinazotoa mikopo ya aina mbalimbali hatua itakayoiwezesha nchi ikiwemo Sekta Binafsi, kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo na kiuchumi.
Mwenyekiti wa Taasisi ya China inayojihusisha na masuala ya Bima-SINOSURE, Mhe. Song Shughuan, akiongoza Ujumbe wa Taasisi yake, walipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), Makao Makuu ya Taasisi mjini Beijing-China, ambapo Tanzania na Taasisi hiyo zimeingia makubaliano yatakayoiwezesha Tanzania kunufaika na huduma za dhamana inayotoa kwa Taasisi za Fedha za China zinazotoa mikopo ya aina mbalimbali hatua itakayoiwezesha nchi ikiwemo Sekta Binafsi, kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo na kiuchumi.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi-Mhe. Prof. Makame Mbarawa (kulia), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed, wakishiriki majadiliano kati ya Taasisi ya Bima ya China-SINOSURE na Tanzania, makao Makuu ya Taasisi hiyo mjinji Beijing China, ambapo Tanzania na Taasisi hiyo zimeingia makubaliano yatakayoiwezesha Tanzania kunufaika na huduma za dhamana inayotoa kwa Taasisi za Fedha za China zinazotoa mikopo ya aina mbalimbali hatua itakayoiwezesha nchi ikiwemo Sekta Binafsi, kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo na kiuchumi.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha-Beijing)
……………………….
Na Benny Mwaipaja, Beijing
Tanzania na Taasisi ya Bima ya SINOSURE ya China zimeingia makubaliano yatakayoiwezesha Tanzania kunufaika na huduma za taasisi hiyo inayotoa dhamana kwa Taasisi za Fedha za China kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa miradi ya uchumi ya serikali na sekta binafsi.
Makubaliano hayo yamefikiwa Mjini Beijing-China, wakati wa ziara ya ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu, ambapo ujumbe huo, pamoja na mambo mengine, una lengo la kuimarisha uhusiano na Taasisi za Fedha za China ili kupata fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa nchini.
Dkt. Nchemba amesema kuwa ushirikiano huo utaimarishwa kupitia nyanja za uwekezaji, biashara pamoja na mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Amesema kuwa hatua hiyo ni matokeo ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini China aliyoifanya Mwezi Novemba mwaka jana ambapo katika mazungumzo yake na Rais wa China-Mhe. Xi Jimping walikubaliana kukuza mahusiano ya kiuchumi katika nyanja mbalimbali.
Dkt. Nchemba alibainisha kuwa mazungumzo na Taasisi hiyo yataiwezesha Serikali na kampuni za Sekta Binafsi kupata dhamana kutoka kwa taasisi ya SINOSURE ili kupata mikopo kutoka kwa taasisi za fedha za China.
Ameeleza kwamba hatua hiyo itasaidia wawekezaji wa China kwenda kuwekeza Tanzania mitaji na teknolojia ambazo zinatasaidia kuharakisha maendeleo ya wananchi na kukuza uchumi kwa ujumla. Vilevile hatua hiyo itawezesha kampuni za China kuuza kwa kampuni za Tanzania bidhaa mbalimbali kwa mkopo kupitia dhamana ya taasisi ya SINOSURE.
“Mazungumzo yetu yamekwenda vizuri na sasa wataalam wa pande zote mbili wameanza majadiliano namna Tanzania inavyoweza kupata fedha kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa njia ya treni ya kisasa-SGR, vipande namba tano hadi saba vinavyoanzia Isaka-Mwanza-Tabora–Kigoma- Uvinza hadi Malagarasi, kwenda hadi nchi Jirani za Burundi na Congo DRC.
Aidha, alisema kuwa mjadala unaendelea ukiwashirikisha wataalam wa pande zote mbili ili kupata fedha za kujenga barabara zenye urefu wa zaidi ya kilometa 2,500 katika mikoa 24 nchini, kutekeleza maelekezo ya Mheshiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anayetaka mikoa yote iunganishwe kwa barabara za lami ili kusisimua uchumi na maisha ya watu kwenye maeneo husika.
Kwa Upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na MIpango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, alisema kuwa uhusiano mwema kati ya Taasisi ya Bima SINOSURE na Tanzania utaiwezesha Zanzibar kunufaika na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Barabara, Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Zanzibar-Terminal IV pamoja na Ujenzi wa Bandari ya Manga Pwani, ambapo mazungumzo na Taasisi hiyo kuhusu kuwezesha upatikanaji wa fedha hizo yanaendelea.
Ziara ya Ujumbe wa Tanzania nchini China katika Taasisi hiyo ya SINOSURE imewashirikisha pia Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi-Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohamed, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Katibu Mkuu-Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Mbelwa Kairuki na viongozi wengine kadhaa waaadamizi wa Serikali.