Na WAF – DSM
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo inaweka Mkakati wa kukabiliana na dharula, magonjwa ya milipuko na matukio yenye athari kiafya yatakayotokea nchini katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Hayo yamebainishwa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu wakati akifungua kikao kazi cha kufanya tathmini jumuishi ya kupima uwezo wa nchi katika kukabiliana na majanga na matukio yenye athari za kiafya kinachofanyika jijini Dar Es Salaam.
“Kikao kazi hiki kina lengo la kujiangalia na kujitathmini kama nchi ni jinsi gani tumeweza kujiandaa kugundua, kukinga na kudhibiti majanga mbalimbali ya kiafya pamoja na magonjwa ya kuambukiza ambayo yanaweza kuikumba nchi na kuleta athari”. Amesema Prof. Nagu.
Prof. Nagu ameongeza kuwa kikao hicho ni moja ya matakwa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo linataka nchi ziweke mkakati wa miaka mitano wa kukabiliana na majanga yanayoweza kutokea na kuleta athari za kiafya kwa wananchi.
Aidha, Prof. Nagu ameongeza kuwa Tanzania ilikua ni nchi ya kwanza kufanyiwa tathmini ya pamoja ya kuangalia uwezo wa nchi katika kukabiliana na matukio yenye athari za kiafya ambapo matokeo ya tathmini hiyo yalionesha kuwa ingawa nchi imekua na maendeleo makubwa bado mapungufu yalikuwepo katika uwezo muhimu wa nchi kuzuia, kugundua na kukabiliana na dharura za afya ya umma.
Naye, Mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Kitengo cha Dharura na Maafa Dkt. Faraja Msemwa amesema kikao hicho ni sehemu ya taratibu za utekelezaji ambapo Shirika hilo linatoa vigezo mbalimbali ambavyo vinatumika katika kufanya tathmini katika kukabiliana na majanga.