Angela Msimbira, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe Angellah Kairuki amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Serikali imedhamiria kuongeza ufanisi na kuboresha elimu nchini kwa kuhakikisha inanunua vitendea kazi kwa maafisa elimu wa Shule za sekondari nchini kwa lengo la kuongeza usimamizi na ufuatiliaji, ufundishaji na ujifunzaji shuleni.
Ameyasema hayo leo Agosti 14, 2023 kwenye hafla ya ugawaji wa magari kwa maafisa elimu sekondari wa Halmashauri nane na Makao Makuu ya Wizara magari mawili iliyofanyika katika shule ya Sekondari ya Azania jijini Dar es Salaam.
Amesema vitendea kazi yakiwemo magari yatasaidia kuongeza ufanisi na kuwawezesha maafisa hao kutekeleza majukumu yao ya kutembelea na kukagua shule, kufuatilia walimu na kusikiliza changamoto badala ya kusubiri wafuatwe ofisini.
”Tunaamini kwamba hakutakuwa na visingizio kwa ninyi kutembelea na kukagua shule, sasa mtaweza kuwafuata walimu na kusikiliza changamoto zao huko huko shuleni kwao badala ya kuwasubiri wawafuate ofisini.”
Mhe. Kairuki ametoa rai kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kusimamia matumizi sahihi ya magari haya na kutenga bajeti za matengenezo.
“Serikali inafanya haya yote ili kutekeleza ILANI ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 Sura ya Tatu Ibara ya 78 inayoelezea Sekta ya Huduma ya Jamii kwa upande wa Elimu.”
Aidha, Mhe. Kairuki ametumia fursa hiyo kuwakumbusha Wakurugenzi hao kusimamia kwa karibu ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari unaoendelea kwenye maeneo yao nchi nzima hasa ya Kidato cha Tano ili wanafunzi wanaporipoti leo tarehe 13 Agosti, 2023 wakute mazingira rafiki ya kujifunzia.
Serikali kupitia Programu ya lipa kulingana na matokeo katika sekta ya elimu (EP4R) imenunua magari 200 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya Maafisa Elimu wa Sekondari wa Halmashauri na ngazi ya Wizara.