Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Nsimbo, Mhe. Anna Lupembe (Mb) imefanya kikao cha hadhara na wananchi wa jimbo la Nsimbo, Wilaya ya Mpanda, Mkoani Katavi.
Kikao hiko kilichofanyika Agosti 12,2023, kililenga kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazohusiana na masuala ya uhifadhi wa maeneo yanayosimamiwa na TAWA katika Kanda ya Magharibi, ikiwemo changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mhe. Anna Lupembe (Mb), alisema mojawapo ya changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo lake ni pamoja na uwepo wa mamba wengi katika Mto Ugalla ambao wamekuwa wakileta madhara kwa wananchi. Vilevile masuala ya ukataji vibali kuwa mbali na makazi ya wananchi, inayosababisha wananchi kutumia gharama kubwa kuvifuata vibali hivyo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu changamoto ya uwepo wa mamba, Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi Nyanda amesema Serikali kwa kushirikiana na Taasisi zake imeweka mikakati ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ikiwemo matumizi ya teknolojia katika kudhibiti wanyamapori hao. Aidha, Kamishna Mabula aliongeza kuwa wanyamapori wanaoleta madhara zaidi kwa wananchi, Serikali imechukua jukumu la kuwaua au kuwavuna ili wasiweze kuleta madhara zaidi.
Kuhusu malalamiko ya wananchi ya kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kukata vibali vya uvuvi na urinaji asali, Kamishna Mabula aliahidi kusogeza huduma ya ukataji vibali kutoka Wilaya ya Mlele hadi Wilaya ya Mpanda kwa ajili ya kurahisisha wananchi kupata huduma hiyo kwa ukaribu zaidi.
Kikao hiki ni muendelezo wa ziara ya Kamishna Mabula katika kutatua changamoto mbalimbali zinazopatikana katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA katika Kanda ya Magharibi