Na John Walter-Ngorongoro
Baadhi ya wananchi wanaoishi ndani ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro katika wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha wamepaza sauti zao kupitia vyombo vya habari wakiwa na Mabango yaliyoandikwa jumbe mbalimbali.
Wananchi hao wakiongozwa na kiongozi wa Kimila wa jamii ya Wamasai Laigwanani Petro Tengesi wamefanya maandamano ya amani katika kijiji cha Kapenjiro wakiwa wamebeba mabango yanayoonesha kuchukizwa na wanaopinga wao kuhamia Msomera.
Wamesema wapo tayari kuhama muda wowote na kwamba wameshafika katika eneo la Msomera kujionea hali ilivyo na kwamba wameridhishwa nayo.
Kiongozi huyo wa mila amesema wamechoka kuishi eneo la Ngorongoro kwa kuwa hawana uhuru wa kufanya shughuli yoyote ya maendeleo kikiwemo kilimo ambacho kingewawezesha kupata chakula.