Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akishiriki Misa Takatifu katika Kanisa Katoliki la Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Parokia ya Kiwanja cha Ndege mkoani Dodoma, Misa iliyoenda sambamba na Maadhimisho ya miaka 47 ya Parokia hiyo leo tarehe 13 Agosti 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na waumini pamoja na viongozi mbalimbali wa dini na serikali mara baada ya kushiriki Misa Takatifu katika Kanisa Katoliki la Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Parokia ya Kiwanja cha Ndege mkoani Dodoma, Misa iliyoenda sambamba na Maadhimisho ya miaka 47 ya Parokia hiyo leo tarehe 13 Agosti 2023.
…….
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewahimiza waumini na Watanzania kwa ujumla kuendelea kufanya kazi kwa bidii katika kilimo, ufugaji, biashara na kutumikia umma kwa uadilifu ili kuchangia katika ujenzi wa Taifa.
Makamu wa Rais ametoa wito huo mara baada ya kushiriki Misa Takatifu katika Kanisa Katoliki la Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Parokia ya Kiwanja cha Ndege mkoani Dodoma, Misa iliyoenda sambamba na Maadhimisho ya miaka 47 ya Parokia hiyo. Amewasihi viongozi wa dini kutokatishwa tamaa na makwazo mbalimbali wanayokutana nayo katika utume wao na kuendelea kuombea jamii na Taifa zima ili Mwenyezi Mungu aendelee kujalia amani na ustawi.
Makamu wa Rais amesema hali ya maadili katika Taifa kwa ujumla hairidhishi ikishuhudiwa kuporomoka kwa maadili na kuongezeka kwa vitendo visivyompendeza Mungu. Ametoa wito kwa wazazi, walezi na walimu kusimamia kiadilifu malezi na makuzi ya watoto na vijana kwa manufaa ya Taifa zima.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka vijana na watoto kuwa na heshima na adabu ili kuweza kukua vizuri na kufanikiwa maishani. Amesema heshima hiyo inapaswa kuwa kwa wazazi, nyumba za ibada, serikali pamoja na mamlaka zingine ambazo zimewekwa na Mungu hapa Duniani.
Katika ibada hiyo pia kumezinduliwa kanisani hapo sanamu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu pamoja na kufanyika kwa sherehe ya kumbukumbu ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Msimamizi na Mwombezi wa Parokia hiyo.
Ibada hiyo imeongezwa na Padre Africanus Kimario akisaidiwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Emmanuel Mutambo na Mapadre wengine na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na serikali.