MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa Ndugu Mohamed Ali Kawaida,akishiriki ujenzi wa Tawi la CCM Tomondo, Wilaya ya Dimani Kichama Unguja.
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa Ndugu Mohamed Ali Kawaida,akiongoza matembezi ya hiari ya kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi,kutoka eneo la Amani hadi Mwanakwerekwe Zanzibar.
………..
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa Ndugu Mohamed Ali Kawaida, amewataka Vijana waliopewa dhamana za kiutendaji ndani Chama na Serikali kufanya kazi kwa bidii ili kwenda sambamba na kasi ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na Viongozi,Watendaji na Wanachama wa UVCCM Mkoa wa Magharibi katika mwendelezo wa ziara yake ya kuimarisha uhai wa Jumuiya hiyo huko Afisi kwao Mwera Unguja.
Alisema kuwa Vijana,wanatakiwa kuwa mfano bora katika masuala mbalimbali ya kujenga Taifa kimaendeleo.
Alisema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha uhai wa Chama na Jumuiya hiyo, kukagua Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2020/2025 na kuhakikisha changamoto zinazowakabili Vijana zinafutiwa ufumbuzi wa kudumu.
” Vingozi wetu Wakuu ambao ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi wametuamini Vijana na kutupatia dhamana mbalimbali hivyo nasi tunatakiwa kuonyesha uwezo wetu kwa vitendo. “,alisema Mwenyekiti huyo Mohamed Kawaida.
Alisema Serikali Kwa Sasa imejielekeza katika kufanya Mapinduzi ya kimaendeleo, kwa kufungua milango ya uwekezaji hasa katika miradi mikubwa ya kimkakati pamoja na Viwanda vitakavyotoa ajira za kudumu kwa Vijana na Wananchi kwa ujumla.
Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo Mohamed, alisema pamoja na juhudi hizo za kuleta maendeleo endelevu nchini bado Kuna makundi ya wanasiasa wasiokuwa wazalendo wanaendelea kubeza na kutoa kauli za kuwachonganisha Wananchi na Serikali zao.
Kupitia Kikao hicho Mohamed Kawaida, aliwapongeza Vijana wa Mkoa huo kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuimarisha Jumuiya na Chama kwa ujumla.
Katika ziara hiyo Mwenyekiti huyo amefuatana na Viongozi wa Kamati tekelezaji ya UVCCM Taifa, Wabunge, Wawakilishi na Wajumbe wa NEC wanaotoka katika Umoja huo.
Mohamed Kawaida ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, katika Mkoa huo amekagua Hospitali ya Wilaya ya Magharib ‘B’, Kukagua Kituo cha Ujasiriamali na UVCCM, kushiriki ujenzi wa Tawi la CCM Tomondo Uzi, kushiriki ujenzi wa Tawi la CCM Bilikani na kuzindua kundi la hamasa la Vijana Fuoni.
Maeneo mengine ni kukagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Polisi Wadi ya Kipungani, maendeleo ya ujenzi wa Soko la Jumbi, kukagua Kituo cha Ujasiriamali Bweleo, kuweka jiwe la msingi katika Maskani ya Maungani, kuongea na Vijana wanaoendesha mradi wa kukusanya takataka pamoja na kufanya majumuisho ya ziara hiyo katika Ofisi za CCM Wilaya ya Dimani Kichama.