Na Selemani Msuya
WADAU 100 kutoka nchi 25 duniani wanakutana jijini Dar es Salaam kwa siku tatu kujadiliana juu ya mbegu za asili ambazo zina mchango mkubwa kwenye usalama na uhakika wa chakula barani Afrika.
Taarifa ya mkutano huo wa aina yake kuhusu mbegu asili imetolewa na Mratibu wa Mtandao na Utunzaji wa Bioanuai Tanzania (TABIO), Abdallah Mkindi wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam.
Mkindi amesema tafiti zinaonesha mbegu asili ni salama na uhakika kwa chakula lakini hazipewi kipaumbele kwenye mfumo wa sera na Sheria na hata kwenye maendeleo ya kilimo.
“Kuanzia Agosti 14 hadi 16 wadau wa mbegu asili zaidi 100 kutoka nchi 25 za Bara la Afrika, Ulaya na Marekani wanakutana jijini Dar es Salaam ajenda kuu ni kuzungumza na kujadiliana juu ya hatma ya mbegu hizo ambazo zinaonekana kutopewa kipaumbele kisera na kisheria,” amesema Mkindi.
Mratibu huyo amesema mkutano wa wadau wa mbegu za asili umeandaliwa na Mtandao wa Uhuru wa Chakula Afrika (AFSA), TABIO na SwissAid.
Amesema Tanzania imepata wenyeji wa kuandaa mkutano huo kwakuwa TABIO ni mwanachama wa AFSA ambayo ina wanachama Africa kote. Amesema katika mkutano huo Tanzania itawakilishwa na TABIO, SwissAid, Bunge, Serikali na taasisi zingine ambazo zipo katika mnyororo wa mbegu na kilimo.
Mkindi ametaja nchi ambazo zitashiriki mkutano huo kuwa ni Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia, Senegali, Burkina Faso, Ivory Cost, Hispania, Norway, Zambia, Zimbabwe na Australia.
“Nyingine ni Togo, Mali, Benin, Chad, Tunisia, Niger, Afrika Kusini, Botswana, Malawi, Misri, Rwanda, DR Congo na Gabon,” amesema.