Bohari ya Dawa (MSD) imejipanga kuboresha huduma zake na kuongeza uwezo wa kuhifadhi bidhaa za afya, ili kuendana na kasi ya serikali ya ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, sambamba na ongezeko la idadi ya watu.
Meneja Miradi Msonge wa MSD, Elias Masumbuko ameeleza hayo wakati wa makabidhiano ya michoro na na eneo baina ya MSD na kampuni ya Hainnan International kwa ajili ya ujenzi wa ghala la kisasa la kuhifadhia dawa kwa ajili ya Kanda ya MSD Mtwara.
“Tumeshuhudia maboresho makubwa ya sekta ya afya chini ya serikali ya awamu ya sita, katika kuongeza vituo vya kutolea huduma za afya ambapo sasa MSD tunatakiwa kuwezesha vifaa na bidhaa za afya kwa vituo hivyo, ili kukamilisha maboresho haya” alisema Bw. Masumbuko
Ameongeza kuwa Kanda ya MSD Mtwara, imekua na ongezeko la vituo vya afya kwa wastani kutoka 592 vya awali hadi kufikia 631, ziko hospitali nyingi zilizofanyiwa maboresho, hivyo kupelekea uhitaji wa kuhuisha uwezo wa Kanda hiyo kuhifadhi bidhaa.
Naye Meneja Miradi wa MSD, Bw. Deo Orauya, amesema kiutaratibu MSD inatakiwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi bidhaa kwa kiwango zinazo tosheleza miezi tisa (9), na kiwango cha chini kwa miezi mitatu (3) lakini kutokana na ufinyu wa ghala la Mtwara, Kanda hiyo inashindwa kuhimili uhifadhi bidhaa hata kwa kiwango cha chini cha miezi 3, na kulazimu magari ya bidhaa kusafiri kila mwezi kuleta bidhaa, hivyo kuongeza gharama za uendeshaji.
Ameongeza kuwa MSD imemkabidhi mkandarasi Hynnan International, eneo lenye ukubwa wa ekari 30, kwa ajili ya ujenzi wa ghala la kisasa lenye ukubwa wa mita za mraba (sqm) 5,000.
Naye Mshauri Mwelekezi wa mradi huo, kampuni ya ABECC, inayomilikiwa na Chuo Kikuu cha Ardhi Dar es salaam, imeahidi weledi katika kushauri na kumsimamia Mkandarasi huyo ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ndani ya muda uliopangwa, ambao mwaka mmoja.