NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Bw. Alex Msama amekerwa na baadhi ya watu wanaomkashifu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suruhu Hassani kupitia mitandao ya kijamii, huku akitoa wito kwa Mamlaka husika kuwachukulia hatua watu wote wanaofanya vitendo hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 12/8/2023 Jijini Dar es Salaam Bw. Msama, amesema kuwa watanzania wanapaswa kumheshimu Mhe. Rais Dkt. Samia, kwani Mwenyezi Mungu ametupa mtu ambaye anaendelea kufanya kazi vizuri kwa manufaa ya Taifa la Tanzania.
“Waache mara moja kumkashifu Mhe. Rais kutokana na kwamba amekuwa anafanya kazi vizuri ili kuhakikisha uchumi wa nchi unaendelea kuimarika, Mhe. Rais ni Mama wa familia kama alivyo mzazi wako, tuache kutoa kauli ambazo sio rafiki” Zinazomdhihaki Rais Dkt. Samia amesema Bw. Msama.
Katika hatua nyengine Bw. Msama ametoa pongezi kwa kamati kuu ya chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kutoa elimu ya uwekezaji kwa watanzania.
Bw. Msama amesema kuwa watanzania wengi wameanza kuwa na uwelewa mkubwa kuhusu uwekezaji kwani baadhi walikuwa wanapotosha watu.
“Wapo baadhi ya watu wanataka kuchafua amani ya nchi yetu, vyombo vya usalama naomba wawachukulie hatua ili kuhakikisha amani ya nchi yetu inaendelea kuwa imara” amesema Bw. Msama.
Amefafanua kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia ameendelea kufanya kazi vizuri ikiwemo kuhakikisha wawekezaji wanaendelea kuwepo nchini.