Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Lazaro Kihalahala kushoto akisaini mkataba wa ujenzi wa kivuko kipya cha Buyagu Mbalika na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Major Songoro kulia katika hafla fupi ya utiaji saini iliyofanyika viwanja vya Sabasaba Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Lazaro Kihalahala kushoto na Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Major songoro wakionyesha mikataba waliyosaini ya ujenzi wa kivuko kipya cha Buyagu Mbalika katika hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba Wilayani Sengerema Mkoani mwanza.Wanaoshuhudia nyuma yao ni Naibu Waziri wa ujenzi Mhe. Godfrey Kasekenya na nyuma ya kihalahala ni Mbunge wa Misungwi Mhe. Alexander Mnyeti na kulia ni Mbunge wa Buchosa Mhe. Erick Shigongo.
…….
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha huduma za usafiri na usafirishaji zinaimarika katika maeneo mbalimbali nchini.Maeneo hayo ni pamoja na anga , nchi kavu pamoja na majini na huku uimarishaji wake ukijikita katika ununuzi na ujenzi wa vifaa vipya na vya kisasa lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za uhakika.
Mathalani, kwa upande wa usafiri wa majini hususan Vivuko, serikali imekuwa ikinunua na kujenga vivuko katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya kanda ya Ziwa ambapo usafiri huu umeonekana kuwa ni mkombozi kwa wananchi wa maeneo hayo.
Kwa kuzingatia hilo , hivi karibuni tumeshuhudia utiaji saini wa mikataba mikubwa ya ujenzi wa vivuko ikiwamo ujenzi wa kivuko kipya cha Buyagu Mbalika jijini Mwanza chenye thamani ya bilioni 3.8, mkataba huo uliosainiwa tarehe 23 Aprili 2023 na kushudiwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi ) Mhe. Godfrey Kasekenya huku Mkandarasi akiwa ni Kampuni ya Kizalendo ya Songoro Marine Transport Limited.
Akiwa katika hafla hiyo, Naibu Waziri Kasekenya alitaja faida za ujenzi wa kivuko hicho kwa kusema kuwa ujenzi utakapokamilika utaharakisha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa wananchi waishio katika Wilaya ya Sengerema, Misungwi na maeneo mengine, aidha inatarajiwa kuwa na usafiri wa uhakika wenye huduma bora na salama katika maeneo ya Buyagu na Mbalika.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Lazaro Kilahala amesema hitaji la kivuko cha uhakika baina ya Buyagu na Mbalika limekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa wananchi wa maeneo hayo hivyo ujenzi wa kivuko hicho utakapokamilika utaondoa kero nyingi za kiuchumi na kijamii ambazo zimekuwa zikichelewesha maendeleo ya wananchi hao hivyo kutimiza azma ya Serikali kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Kilahala ameeleza kuwa katika mwaka huu wa fedha, Wakala unaendelea na ujenzi wa vivuko vipya vitano vyenye thamani jumla ya Bilioni 33.2 vitakavyotoa huduma kwenye vituo vya Kisorya – Rugezi, Bwiro – Bukondo, Nyakarilo – Kome, Ijinga – Kahangala na Mafia – Nyamisati hivyo kivuko cha Buyagu-Mbalika ambacho leo mkataba wake wa Ujenzi umesainiwa ni kivuko cha sita (6) ambacho Ujenzi wake unaanza katika mwaka huu wa fedha.
Aliongeza kuwa sambamba na Ujenzi wa vivuko vipya katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali kupitia Wakala inafanya ukarabati wa vivuko 18 pamoja na Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vivuko katika maeneo 11 ya huduma kwa gharama ya bilioni 27.5.
Halikadhalika, mapema mwaka huu Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya alipata wasaa wa kukagua karakana ya ujenzi wa meli na vivuko ya Songoro jijini Mwanza na kupata taarifa ya maendeleo ya ujenzi na ukarabati wa vivuko hivyo vitakavyogharimu takribani bilioni 26 na kutarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Agosti mwaka huu.
Aidha, Imeelezwa kuwa kukamilika kwa ujenzi wa vivuko vipya vinne na ukarabati wa vivuko vinne vitakavyotoa huduma katika maeneo mbalimbali ya Ziwa Victoria kutapunguza changamoto za usafiri kwa wananchi wanaoishi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na kutarahisisha shughuli za maisha kwa urahisi, uhakika na usalama.
Naye, Kaimu Meneja Vivuko Kanda ya Ziwa na Magharibi kutoka TEMESA Mhandisi, Aloyce Ndunguru, alisema kuwa wanaendelea na ujenzi wa vituo vipya vitatu ambavyo ni Bwiro (kisiwani) – Bukondo katika Wilaya ya Ukerewe, Kituo cha Ijinga (kisiwani) – Kahangala katika Wilaya ya Magu na Kituo cha Mayenzi – Kanyinya ambapo miradi hiyo ikikamilika itafanya wawe na jumla ya vituo 16 katika kanda hiyo.
Alieleza pia kanda hiyo ina jumla ya vivuko 17 ambapo kati ya hivyo vivuko vinne vipo katika matengenezo makubwa ambavyo ni MV Misungwi (Kigongo – Busisi), MV Mara (Iramba – Majita), MV Ujenzi (Kisorya – Rugezi) na MV Nyerere (Bugolora – Ukara).
Katika bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/2024 mradi wa ujenzi na ukarabati wa vivuko na maegesho ya vivuko, umetengewa jumla ya shilingi bilioni 14.3 ambapo mradi wa ujenzi wa vivuko vipya umetengewa bilioni 5.7 kwa ajili ya ununuzi wa vivuko vipya vya Kisorya-Rugezi, Ijinga – Kahalanga, Bwiro-Bukondo, Nyakarilo – Kome, Nyamisati – Mafia na Buyagu – Mbalika.Kazi nyingine ni ununuzi wa boti mbili ndogo (Sea taxi ferries) zitakazotoa huduma katika kituo cha Magogoni- Kigamboni , ununuzi wa vifaa vya karakana za TEMESA, huduma za ushauri pamoja na usimamizi na ufuatiliaji wa miradi hiyo.
Pia mradi wa kukarabati wa vivuko umetengewa jumla ya bilioni 6,089 kwa ajili ya kukamilisha ukarabati wa kivuko Mv Ujenzi, Mv Mara,Mv Kome II, Mv Malagarasi, Mv Mafanikio, Mv Misungwi , Mv Nyerere,Mv Kyanyabasa, Mv Tanga na Mv Kitunda.
Aidha kazi nyingine ni kuanza ukarabati wa vivuko Mv Mwanza, Mv Kigamboni, Mv Ukara 1, Mv Ukara II, Mv sabasaba , Mv Pangani II na ukarabati wa boti ya uokozi ya Mv SAR II , ukarabati wa kivuko Mv Kilombero II na kukihamisha kwenda Mlimba- Malinyi pamoja na ufuatiliaji wa tathmini ya miradi hiyo.
Ni dhahiri kuwa Serikali imejizatiti vya kutosha kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora za usafiri na usafirishaji zinazochochea ukuaji wa uchumi, ni wajibu wetu sisi kama wananchi kuhakikisha tunatunza vyema rasilimali zetu na kuzilinda kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.