Waziri Wa Nishati Mhe. January Makamba (kulia) na Waziri wa Nishati nchini Malawi Mhe. Ibrahim Matola wakishika hati ya makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya Nishati baada ya kusaini katika Hafla iliyofanyika leo Agosti 11, 2023 Jijini Dar es Salaam.
Waziri Wa Nishati Mhe. January Makamba akisani Makubaliano ya Ushirikiano na nchi ya Malawi katika Sekta ya Nishati katika hafla iliyofanyika leo Agosti 11, 2023 Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati nchini Malawi Mhe. Ibrahim Matola akisani Makubaliano ya Ushirikiano na nchi ya Tanzania katika Sekta ya Nishati katika hafla iliyofanyika leo Agosti 11, 2023 Jijini Dar es Salaam.
Waziri Wa Nishati Mhe. January Makamba (kulia) na Waziri wa Nishati nchini Malawi Mhe. Ibrahim Matola wakishikana mikono kama ishara ya kupongezana baada ya kusaini Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya Nishati baada ya kusaini katika Hafla iliyofanyika leo Agosti 11, 2023 Jijini Dar es Salaam.
Mawaziri wa Nishati wa Tanzania na Malawi wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali walioshiriki katika hafla ya kusaini Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Nishati.
Waziri wa Nishati nchini Malawi Mhe. Ibrahim Matola (wa pili kulia) akizungumza jambo alipotembelea leo Agosti 11, 2023 mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi II uliopo eneo la Kinyerezi Jijini Dar es Salaam l
Waziri wa Nishati nchini Malawi Mhe. Ibrahim Matola akiwa na wataalamu wake akiangalia mitambo ya kuzalisha umeme wa Kinyerezi II uliopo eneo la Kinyerezi Jijini Dar es Salaam
……….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeingia makubaliano ya ushirikiano na Nchi ya Malawi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya pamoja katika sekta ya Nishati ikiwemo kuzalisha umeme Megawatts 300 kupitia nguvu ya maji katika Mto Songwe.
Akizungumza leo Agosti 10, 2023 Jijini Dar es Salaam katika hafla ya kusaini Makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi, Waziri Wa Nishati Mhe. January Makamba, amesema kuwa amesaini makubaliano mawili katika sekta ya nishati pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Malawi.
Mhe. Makamba amesema kuwa makubaliano hayo yapo katika maeneo makubwa matatu ambayo ni kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji katika mto Songwe ambao upo katika nchi mbili Tanzania na Malawi.
“Tumeamua tufanye mradi huo kwa pamoja, pia tutashirikiana katika kufanya utafiti, uchimbaji wa gesi, mafuta pamoja na ujenzi wa miundombinu ya umeme” amesema Mhe. Makamba.
Amesema kuwa katika utekelezaji wa makubaliano wameweka utaratibu wa ushirikiano kwa kuunda kamati ya pamoja ya mawaziri na kamati ya wataalamu ya kufatilia utekelezaji.
Mhe. Makamba amesema kuwa kila nchi itateuwa wataalamu ndani ya mwezi mmoja, huku akieleza kuwa vikao rasmi vya utekelezaji vinatarajia kuanza October mwaka huu.
“Tunafanya mradi huu kutokana na umuhimu wa utekelezaji wa pamoja katika sekta ya nishati, pia ni maelekezo ya viongozi wetu Rais wa Tanzania na Malawi” amesema Mhe. Makamba.
Amesema kuwa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya umeme ni sehemu ya kuwa na gridi moja katika eneo la Kusini mwa Afrika.
Amefafanua kuwa mpaka sasa Tanzania ina miradi kadhaa ya kuunganisha na nchi nyengine ambapo tayari wamekamilisha manunuzi ya kuunganisha gridi yaTanzania na Zambia na kwenda Kusini mwa Afrika.
“Huu ni sehemu ya mradi wa kikanda katika kuhakikisha kunakuwa na kanda moja katika gridi hii, tayari makatibu wakuu na wataalamu walizungumza na leo tumefanya ngazi ya mawaziri” amesema Mhe. Makamba.
Amesema kuwa mradi unakwenda kunufaisha nchi ya Tanzania na Malawi katokana mahitaji ya umeme bado ni makubwa katika uzalishaji mali na huduma za kijamii.
Waziri wa Nishati nchini Malawi Mhe. Ibrahim Matola, amesema kuwa ushirikiano huo unakwenda kuleta tija katika kuleta maendeleo baini ya nchi mbili.
Mhe. Matola amesema kuwa ni muhimu kufanya uwekezaji wa pamoja katika sekta ya nishati ikiwemo kuzalisha umeme ambao mahitaji yake bado ni makubwa.
Hata hivyo baada ya kusaini Makubaliano ya Ushirikiano Waziri wa Nishati Mhe. Matola akiwa na timu yake wametembelea mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi II uliopo eneo la Kinyerezi Jijini Dar es Salaam