Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ruru wilayani Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua athari za magugu maji hayo katika Ziwa Jipe leo Agosti 10, 2023.
Mkuu wa Wilaya Mwanga Mhe. Abdallah Mwaipaya akifafanua jambo wakati wa ziara ya Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ya kukagua athari za magugu maji hayo katika Ziwa Jipe leo Agosti 10, 2023.
…….
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali inaendelea kushughulikia changamoto ya kuwepo kwa magugu maji katika Ziwa Jipe lililopo wilayani mkoani Kilimanjaro.
Mhe. Khamis amesema hayo alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua athari za magugu maji hayo katika ziwa hilo lililopo Kijiji cha Ruru wilayani humo leo Agosti 10, 2023.
Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho amesema kuwa Serikali bado inatambua changamoto hiyo na hivyo itahakikisha magugu maji hayo yanaondolewa.
Amebainisha kuwa Serikali imeshaandika andiko lenye thamani ya shilingi bilioni 18 na kuwasilisha kwa wahisani ili waweze kufadhili mradi wa kuondoa magugu maji hayo.
Naibu Waziri Khamis amewahakikishia wananchi hao kuwa mara fedha hizo zitakapopatikana, Serikali itaanza kutekeleza mradi huo mara moja ili kukabili changamoto hiyo.
Aidha, amewataka wananchi wa Kata ya Jipe na maeneo yote yanayozunguka ziwa hilo kuhakikisha wanatunza mazingira ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame wa muda mrefu.
“Ndugu zangu tuendelee kupanda miti ya kutosha pamoja kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu pembezoni mwa ziwa hili ili tulinusuru na athari za kimazingira,“ amesisitiza.
Ziwa Jipe ambalo limezungukwa na Kenya na Tanzania likiwa ukubwa wa kilomita za mraba 30 linasaidia maisha ya wananchi wa Tanzania takriban 3222 kwenye shughuli za uvuvi, kilimo, ufugaji na uhifadhi wa bionuwai pamoja na shughuli za utalii.
Inaelezwa kuwa shughuli za uvuvi zimepungua kwa kiasi kikubwa kwenye ziwa hilo kutokana na magugu maji yaliyoota ziwani haswa upande wa Tanzania hali iliyosababisha Serikali kufanya jitihada za kuondoa magugu maji hayo.