Na Victor Masangu,Kibaha
Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Selina Koka katika Kuhakikisha anaweka misingi imara ya kukiimarisha chama cha mapinduzi (CCM) amegawa vitendea kazi mbali mbali kwa kata zote 14 kwa ajili ya matumizi ya ofisi za jumuiya ya umoja wa wazazi katika Wilaya ya Kibaha mjini.
Selina ambaye pia ni mlezi wa jumuiya ya umoja wa wazazi Kibaha mji alisema kwamba ameamua kutoa vifaa hivyo vya steshenari kwa lengo la kuwarahisishia wenyeviti na makatibu kufanya kazi za chama kwa lengo la kuwasaidia wanachama wao.
Hayo yamebainishwa katika mafunzo ya jumuiya ya umoja wazazi ngazi ya kata ambayo yamefanyika katika ukumbi wa halmashauri ya mji kibaha na kuhudhuliwa na viongozi mbali mbali wa chama pamoja na mumeo Silvestry Koka ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini.
“Leo nimefurahi sana kushiriki katika mafunzo haya ya jumuiya ya wazazi lakini pamoja na hayo niliahidi kuboresha vitendea kazi katika ofisi zote 14 zilizopo ndani ya jimbo la Kibaha kwa hiyo nina imani kubwa vifaa hivi vya steshenari vitawasaidia viongozi katika utekelezaji wa majukumu yao,”alisema Selina.
Aidha Selina aliahidi kuendelea kuwasaidia wanawake kiuchumi kwa kuwapatia mitaji pamoja na mafunzo mbali mbali ili kuweza kuondokana na wimbi la umasikini lengo ikiwa ni kuwaletea maendeleo wanawake.
Aidha aliongeza kuwa viongozi wanapswa kumpa ushirikiano Rais wa awamu ya sita Samia Suluhu Hassan,pamoja na Mbunge wa jimbo la Kibaha mjini kuendelea kuwapa muda katika kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu yao bila kusumbuliwa kwa maslahi ya wananchi.
Kwa Upande wake mmoja ya wakufunzi wa mafunzo hayo Abdalah Zaidi amewataka viongozi hao kuhakikisha wanasimamia malezi kwa watoto wao ili kuepukana na changamoto ya kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili.
“Mafunzo haya yataweza kuwasaidia zaidi viongozi wa kata zote 14 za jimbo la Kibaha mjini kwa hiyo kikubwa ninachoomba ni kusimamia maadili hasa kwa watoto wetu ikiwemo mambo ya ushoga,”alisena Zaidi.
Pia mkufunzi huyo ambaye ni kada wa CCM kutoka Wilaya ya bagamoyo aliwakunbusha viongozi hao kuachana na tabia ya kutoa siri za chama na badala yake wabadilike na kuweka mikakati ya kukiimarisha chama pamoja na kukilinda.
“Ni wajibu wa kila kamati ambazo zitaundwa katika jumuiya ni kulinda Siri za chama katika ngazi mbali mbali kuanzia matawi,mashina na kuendelea na kufanya hivyo kutaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kulinda maadili ya wanachama wote,”alisena mkufunzi huyo.
Katika hatua nyingine alimpongeza Mbunge wa jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka kwa kutekeleza ilani ya chama kwa vitendo na kuwataka baadhi ya watu kuachana na vitendo vya kuwaingilia viongozi waliopo madarakani na badala yake wawape ushirikiano wa kutosha mpaka wamalize muda wao.
Jumuiya ya umoja wa wazazi Wilaya ya Kibaha mji imeamua kuwapatia mafunzo mbali mbali viongozi wa ngazi za kata zote 14 kwa lengo la kuwakumbusha mambo mbali mbali ikiwemo maadili,itifaki,majukumu na wajibu wa viongozi pamoja na mambo mengine.