Na Mwandishi wetu, Simanjiro
DIWANI wa Kata ya Loiborsoit Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Siria Baraka Kiduya, amesoma taarifa ya maendeleo na changamoto zilizopo kwenye eneo lake katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Akisoma taarifa hiyo Kiduya amesema Kata ya Loiborsoit ina vijiji viwili ambavyo ni kijiji cha Ngage na Loiborsoit B, Kijiji cha Ngage, Vitongoji vyake ni Ngage A, Ngage B na Ndepes na Kijiji cha Loiborsoit B ina vitongoji vya Engurush, Oltibu na Mazinde.
Amesema Kata Loiborsoit imepakana na Kata zifuatazo, ambapo kaskazini imepakana na kata ya Ngorika, kusini ni Kata ya Ruvu Remit, mashariki mto Pangani na magharibi ni kata ya Endonyongijape na na Kijiji cha Najuu Kata ya Langai.
Diwani huyo amesema kuhusu taarifa ya mimba na utono ni kuwa kwa kipindi cha mwezi March hadi Julai, hakuna mimba zilizoripotiwa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kata ya Loiborsoit.
“Utoro umedhibitiwa kwa kiasi kikubwa na utoro sugu umeisha kwa kiwango kikubwa kwani wanafunzi wanahudhuria masomo kwa asilimia 95,” amesema Diwani Kiduya.
“Pia tumefanikiwa kuanza ujenzi wa nyumba moja ya walimu ya two in one kwenye shule ya msingi Losokoni ila wananchi wanaomba kusogezewa huduma za kituo cha afya,” amesema Diwani Kiduya.
Ametaja miradi mingine ni Loiborsoit “B, ujenzi wa josho (Nengaron), ujenzi bado unaendelea na gharama yake ni shilingi milioni 23, ujenzi wa Wando inteck (Chamamba) na mfereji wa Malila, gharama yake ni shilingi milioni 16.6 na tayari vifaa vipo site.
Diwani Kiduya amesema Kata ya Loiborsoit ina jumla ya idadi ya wafugaji 650 na ina idadi ya mifugo 46,875 wakiwemo ng’ombe 24,924 mbuzi 10,800 kondoo 10,095 na punda 1,056.
Amesema bei ya mazao ni nzuri kwa pande zote za mazao ya vitunguu, mahindi na mpunga na pembejeo za ruzuku inaendelea kutolewa kwa kipindi chote na vile vile usajili wa wakulima unaendelea kwa kipindi cha 2022 – 2023 na 2023 – 2024.
Hata hivyo, Diwani huyo ametaja changamoto ya kuwepo na magonjwa ya mlipuko kwenye zao la mpunga (RMV), njia za mashambani za kutolea mazao pamoja na vivuko (madaraja).
“Mheshimiwa Mwenyekiti bado tuna mgogoro na Kata ya Endonyongijape kuendeleza eneo la Kata ya Loiborsoit tunaomba tusaidiwe kutatua mgogoro huu,” amesema Kiduya.
Ametaja changamoto nyingine ni ukosefu wa barabara, ukosefu wa umeme baadhi ya maeneo Ndepes, Jangwani, Songoyo, Kwasakwasa na Mangulai.
Amesema pia kwenye eneo hilo wanakabiliwa na changamoto ya daraja linalounganisha Wilaya ya Simanjiro na Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro.
“Pia mifugo mingi kufa kutokana na ukame, ukosefu wa majosho hali inayosababisha mifugo mingi kuathirika kutokana na magonjwa yanayosababishwa na kupe,” amesema Diwani Kiduya.
Amesema pia kuna upungufu wa walimu wa kike shule ya msingi Loiborsoit “B” na Mazinde, upungufu wa madarasa shule ya msingi Ngage 2, Ndepes 4, Loiborsoit “B” 2 na Mazinde 2.