Askofu wa Kanisa la TAG Igombe Rodrick Shoo akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhi sare za shule kwa wanafunzi.
Maratibu wa asasi za kiraia Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Yusuph Omollo akikabidhi sare za shule kwa mwanafunzi.
Wanafunzi kutoka shule za msingi zilizopo katika Kata ya Bugogwa wakiwa wamevalia sare za shule walizokabidhiwa na Askofu wa Kanisa la TAG Igombe.
Wanafunzi,walimu na wazazi wakiwa kwenye hafla fupi ya kukabidhiwa sare za shule katika kanisa la TAG.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Igombe lililopo mtaa wa Kigote Kata ya Bugogwa Wilaya ya Ilemela Mkoani mwanza limetoa sare za shule kwa wanafunzi 250 zenye thamani ya milioni tano lengo ikiwa ni kuwatia moyo ili waweze kutimiza ndoto zao.
Akizungumza leo Alhamisi Agosti 10, 2023 kwenye hafla fupi ya kukabidhi sare hizo Askofu wa TAG Jimbo la Mwanza Kaskazini Rodrick Shoo amesema wametoa sare hizo ili watoto wenye nia ya kusoma wasishindwe kwasababu ya kukosa sare za shule.
Askofu Shoo ameeleza kuwa mbali na kuwapa sare za shule wamekuwa wakifanya ukarabati wa vyoo vya shule katika shule za msingi ili kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira rafiki na salama.
“Tulikarabati vyoo katika shule ya msingi Bugogwa, kisundu,Igombe na mwaka huu tumekamilisha ukarabati wa vyoo katika sekondari ya Bugogwa”, amesema Askofu Shoo
Ameeleza kuwa wanalengo la kujisajili ili wawe na taasisi inayojitegemea itakayoruhusu kufungua milango mikubwa ya watu kuungana nao ili kwa pamoja wakabiliane na changamoto ya watoto kukosa sare za shule.
Kwa upande wake Afisa elimu Kata ya Bugogwa Clavery Kazilo, amesema kitendo cha wanafunzi hao kupewa sare za shule ni uzalendo mkubwa sana unaosaidia kupunguza ukatili pindi wanapokuwa shule.
“Wanafunzi wanatoka katika mazingira tofauti tofauti kunawanao toka kwenye familia tajiri na wengine familia masikini hivyo mtoto anapovaa sare iliyochanika wenzake wakamcheka anakuwa amefanyiwa ukatili ambao utamfanya aichukie shule hivyo kanisa hili la TAG Igombe limefanya jambo zuri na linastahili kuigwa na taasisi zingine”, amesema Kazilo.
Erasto Fred ni Mwalimu Mkuu shule ya msingi Kayenzendogo ameeleza kuwa mwanafunzi anapokuwa amevaa sare za shule nzuri inasaidia kuchochea uelewa darasani lakini anapokuwa amevaa ambazo zimechanika zinamfanya ashindwe kujiamini na kuacha kuja shule kabisa.
Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Kigote Maungo Malima amesema wazazi wajitahidi kuwahimiza watoto wao kwenda shule kwani baadhi yao wanakataa shule bila sababu za msingi na hivyo kushindwa kutimiza ndoto zao.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Mratibu wa asasi za kiraia Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Yusuph Omollo, amewataka wanafunzi waliopewa sare za shule kuzitunza vizuri ili ziweze kuwasukuma kwa muda mrefu huku akiongeza kuwa wanafunzi wanaposoma katika mazingira mazuri inasaidia kuwa na ufauli mzuri darasani.