1. Ni TASAF usipime, kazi inatufanyia,
Matunda yake tusome, tuzidi kufurahia,
Mfuko huu uvume, jinsi unasaidia,
Lightness Mwasano, yake yanatuingia.
2. Alikuwa na wazazi, ambao lijivunia,
Baba kapata makazi, kifo kilipomjia,
Huku mama hana kazi, TASAF ikaingia,
Lightness Mwasano, yake yanatuingia.
3. Sana imesaidia, tuko alikoanzia,
Elimu kumlipia, ngazi akijipandia,
Mara mama yake pia, kifo kikamwangukia,
Lightness Mwasano, yake yanatuingia.
4. Pasipo hii TASAF, yeye kumsaidia,
Asingezivuka safu, pazuri akafikia,
Yeye nasi twaisifu, yale imemfanyia,
Lightness Mwasano, yake yanatuingia.
5. Na wadogo zake pia, TASAF yasaidia,
Maisha wanapitia, adha yawapunguzia,
Hapahapa Tanzania, mfuko twajivunia,
Lightness Mwasano, yake yanatuingia.
6. Elimu alofikia, shahada nakuambia,
TASAF afurahia, ilivyomsaidia,
Kero kumpunguzia, ushuhuda atwambia,
Lightness Mwasano, yake yanatuingia.
7. Huyu ni mmoja mtu, TASAF ajivunia,
Wako wengi wengi watu, kwenye yetu Tanzania,
Tasaf mefanya vitu, wote wanashangilia,
Lightness Mwasano, yake yanatuingia.
8. Kazi ni maendeleo, kwa watu wa Tanzania,
Hakuna upendeleo, Mfuko wafwatilia,
Kuna mengi matokeo, wale wanautumia,
Lightness Mwasano, yake yanatuingia.
9. Serikali za Mitaa, zidisha kusaidia,
Huko kwenu mnakaa, watu mwawaangalia,
Wahitaji wachakaa, TASAF yasaidia,
Lightness Mwasano, yake yametuingia.
10. Wanyonge kusaidia, dini safi nakwambia,
TASAF twashangilia, ndivyo inatufanyia,
Hongera twawapatia, mnatukuna sikia,
Lightness Mwasano, yake yametuingia.
11. TASAF toka zamani, vyema inatufanyia,
Mfano bora nchini, matunda twajipatia,
Heko na Serikalini, misuli kuipatia,
Lightness Mwasano, yake yametuingia.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
[email protected] 0767223602